Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Oktoba 06, 2024 Local time: 01:01

Balozi za Ulaya zatoa tahadhari kuhusu tishio la shambulizi la kigaidi Kenya


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Idara za usalama nchini Kenya zinafuatilia kwa karibu masuala ya usalama baada ya balozi za Ulaya kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa shambulizi la kigaidi katika miji mikubwa nchini humo.

Balozi za Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi zimewatahadharisha raia wake dhidi ya uwezekano wa shambulizi la kigaidi katika mji mkuu Nairobi.

Kwenye tahadhari hiyo mataifa hayo yamewashauri raia wao kuepuka maeneo ya starehe na kwenye mikusanyiko ya watu.

Uingereza nayo imewaonya raia wake kuepuka safari zisizo za lazima na kutosafiri katika baadhi ya maeneo kama vile huko jimbo la Garissa na maeneo yote mpaka wa Kenya na Somalia.

Maeneo mengine yaliyotajwa ni pamoja na Mandera, Tana River na Mpeketoni.

Msemaji wa Polisi Bruno Shioso katika taarifa yake amewahakikishia Wakenya kuwa vikosi mbali mbali vya usalama vimeimarisha doria kukabiliana na tukio lolote.

Idara hiyo ya polisi imewasihi Wakenya kuwa waangalifu ili kutambua tishio lolote.

Rais Uhuru Kenyatta amekutana na makamanda wa vitengo mbali vya polisi nchini humo pamoja na makamishna wa kaunti leo Ijumaa kuangazia hali ya usalama.

Msemaji wa ikulu ya rais Kanze Dena katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amesema kuwa mkutano huo ulilenga kuangazia hali ya usalama wa taifa.

Mapema wiki hii waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiang'i alikutana na wakuu hao, ambapo suala la mashambulizi ya al- Shabaab katika eneo la Lamu lilijadiliwa.

Matian’gi alisema ingawa kumekuwepo na mafanikio katika kukabiliana na makundi ya kigaidi juhudi zaidi zinahitajika kupambana na kundi hilo ikiwemo kuimarisha doria.

Jumatano wiki hii maafisa 5 akiwemo hakimu wa mahakama ya kuhama hama katika jimbo la Lamu Paul Rotichwalishambuliwa kwa bunduki na washukiwa 6 wa kundi la al-Shabaab.

Kufikia sasa takriban watu 15 wamepoteza maisha baada ya mashambulizi ya al-Shabaab mwaka huu wa 2022, washukiwa 10 wakizuiliwa na polisi kwa kuhusika na mauaji hayo.

Hata hivyo wanamgambo hao wameendelea kushambulia maeneo mbali mbali licha ya uwepo mkubwa wa maafisa wa usalama.

Shule kadhaa hazijafunguliwa wanafunzi wakihofia usalama wao huku jimbo hilo likiwa chini ya marufuku ya kutotok nje usiku.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Collins Liberty Adede, Mombasa, Kenya

XS
SM
MD
LG