Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 05:38

Al-Shabab yatoa tishio jipya dhidi ya Kenya


Vyombo vya usalama na watu wengine wakipita mbele ya Hotel Hayat iliyoharibiwa na shambulizi la kigaidi mjini Mogadishu, Somalia, Aug. 21, 2022.
Vyombo vya usalama na watu wengine wakipita mbele ya Hotel Hayat iliyoharibiwa na shambulizi la kigaidi mjini Mogadishu, Somalia, Aug. 21, 2022.

Kikundi cha wanamgambo wa Kiislam al-Shabab cha nchini Somalia chenye uhusiano na al-Qaida wametoa tishio jipya dhidi ya nchi jirani ya Kenya.

Kikundi hicho kimesema kitaendeleza mashambulizi katika nchi hiyo kwa kipindi ambacho wanajeshi wa Kenya wataendelea kuwepo Somalia.

Al-Shabab ilisema katika tamko lake kwa lugha ya Kiingereza Jumamosi itaendelea kulenga mashambulizi yake katika miji midogo na mikubwa ya Kenya mpaka wanajeshi wa Kenya waondoke Somalia.

Imesema kama serikali ya Kenya itaendelea kudumisha “uvamizi” wake kwenye ardhi za Waislam itaendelea kufanya mashambulizi ndani ya Kenya.

“Mtambue kuwa tutaendelea kuitetea ardhi yetu na watu wetu kutokana na uvamizi wa kichokozi wa Kenya. Tutaendelea kuelekeza kwa nguvu zote mashambulizi katika miji midogo na mikubwa ya Kenya muda wa kuwa majeshi ya Kenya yataendelea na uvamizi wa ardhi za Waislam,” kikundi hicho kilisema.

Omar Mahmood, mtafiti wa ngazi ya juu wa kikundi cha International Crisis kwa Mashariki mwa Afrika alijadili hali hiyo na VOA kupitia mtandao wa WhatsApp.

“Kwa ujumla, al-Shabab imebakia kuwa tishio kwa Kenya, kwa pande zote kupitia mpakani na mashambulizi ya kigaidi katika sehemu nyingine za nchi hiyo. Hivyo basi, wataendelea kujaribu kuilenga Kenya iwapo hawatapata kile wanachokitaka, ambacho msingi wake ni kusitishwa kabisa operesheni za kijeshi za Kenya nchini Somalia,” alisema.

Mohamed Husein Gaas, mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Raad Peace yenye makao yake Mogadishu, aliiambia VOA kwa njia ya simu kuwa tishio la al-Shabab ni la kweli, kama walivyoshuhudia kikundi hicho kikiwa na uwezo zaidi wa kifedha katika miaka michache iliyopita, licha ya kuwepo majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia.

“Eneo hilo liliongezeka kuwa hatarini kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia na migawanyiko ya kisiasa na kijamii iliyokuwepo inayoweza kuongeza ukosefu wa usalama wa eneo hilo kwa ujumla,” alisema.

Alisema kikundi hicho pia kinaweza kuwa kimepata uzoefu wa kupanua himaya yake, kama ilivyoshuhudiwa katika mashambulizi ya hivi karibuni katika jimbo la Somalia nchini Ethiopia.

Al-Shabab wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Somalia na operesheni zaulinzi wa amani wa AU kwa zaidi ya miaka 15.

XS
SM
MD
LG