Emine Dzhaparova amekiambia kituo cha utangazaji cha CNBC TV 18 katika mahojiano kuwa Kyiv pia inatarajia India kuwakaribisha maafisa wa Ukraine kushiriki katika matukio ya G-20 na kuongeza mazungumzo ya kisiasa na Kyiv.
India inashikilia urais unaozunguka wa Kundi la G-20 mwaka huu na ni mwenyeji wa mkutano wa viongozi utakaofanyika Septemba.
Emine Dzhaparova
New Delhi haijakuwa mkosoaji wa Moscow kama nchi nyingine zinavyokosoa uvamizi wa Russia nchini Ukraine na pia imeongeza ununuzi wa mafuta ya Russia – ikiwa ni uhai wa uchumi wake – wakati wengine wamekuwa wakinunua mafuta kidogo au kupiga marufuku.
Dzhaparova, ambaye yuko New Delhi kwa ziara ya siku nne, alimwambia mtangazaji: “Sisi tunaamini India inalazimika kujihusisha na kuwasiliana juu ya suala la Ukraine kwa kiwango kikubwa zaidi.
“Tunaamini kuweka uzito zaidi kwa mdahalo wa kisiasa katika ngazi ya juu kabisa ni hatua ya kwanza kufikia hili lengo kubwa. Rais wangu anaomba kuwa na mazungumzo ya simu na waziri mkuu. Tunashauku ya kumkaribisha Kyiv siku moja,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, alisema India ni lazima iwe na msukumo katika kuhifadhi rasilmali zake, ikiwemo nishati na vifaa vya ulinzi, huku akiitahadharisha juu ya kuitegemea Russia.
India imeendelea kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa vita nchini Ukraine, wakati Modi alimwambia Rais wa Russia Vladimir Putin mwezi Septemba kuwa hivi sasa “siyo zama za vita.”
India pia imeboresha ununuzi wake wa mafuta ya Russia, ikitumia fursa ya unafuu wa juu wa bei ya mafuta kufuatia marufuku ya manunuzi ya mafuta iliyowekwa na Umoja wa Ulaya
Russia, kama ilivyokuwa Umoja wa Sovieti kabla yake, imekuwa ni chanzo kikuu kwa India cha manunuzi yake ya silaha na vifaa vya ulinzi na hivi sasa imeifanya Russia ichukue nafasi ya Iraq kama ni muuzaji mkuu wa mafuta ghafi kwa India.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters