Mshukiwa huyo Philip Manhaus raia wa Norway, 21, alifikishwa mahakamani nchini humo akionekana amejeruhiwa jicho moja huku akiwa anatabasamu.
Mtu huyo anakabiliwa na mashtaka ya mauaji na jaribio la mauaji. Hakuna mtu aliyeuwawa ndani ya msikiti huo, lakini saa chache baadae polisi waligundua maiti ya dada wa kambo wa mshukiwa katika eneo jingine na anatuhumiwa kwa mauaji hayo.
Polisi ya Norway inaliangalia tukio hilo la Jumapili la mtu huyo kutaka kushambulia kwa risasi msikiti huo kama jaribio la kigaidi.
Naibu Mkuu wa Polisi wa mji wa Oslo Rune Skjold amesema polisi wamepata ushahidi kuwa mshukiwa alikuwa na maoni makali ya mrengo wa kulia, na inashukiwa kwamba alikuwa na chuki dhidi ya wahamiaji.
Jumapili, mshukiwa alianza kuwarushia risasi watu wawili kwenye msikiti huo, lakini baadae alidhibitiwa na mzee wa miaka 65 ambaye ni afisa wa zamani katika jeshi la anga la Pakistani.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.