Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 17, 2024 Local time: 18:10

Watu 20 wauawa katika shambulizi la risasi El Paso, Texas


Shambulizi la El Paso, Texas.
Shambulizi la El Paso, Texas.

Watu 20 waliuawa na wengine zaidi ya 26 kujeruhiwa kwenye shambulizi la risasi katika mji wa El Paso, Texas, Jumamosi asubuhi.

Kwa mujibu wa polisi, mtu aliyekuwa amejihami na bunduki alianza kuwashambulia kiholela wateja kwenye eneo la kuegesha magari nje ya duka la Celo Vista Walmart, kabla ya kuingia ndani, ambako kulikuwa na zaidi ya wateja 1,000 na wafanyakazi kadhaa na kuanza kuwashambulia.

Mshukiwa huyo, ambaye alikamatwa na polisi muda mfupi baadaye, alitambulishwa kama Patrick Crusius, mwanamme mzungu mwenye umri wa miaka 21 na anayetokea mjini Allen, Texas.

Rais Donald Trump alisema kupitia ujumbe wa Twitter kwamba analaani kitendo hicho.

"Hakuna sababu au kisingizio chochote cha kuwaua raia wasio na hatia. Melania na mimi tunatuma rambirambi za dhati na maombi kwa niaba ya watu wa jimbo tukufu la Texas," Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mgombea urais Beto O'Rouke, ambaye ni mwenyeji wa eneo la tukio, aliwaambia waandishi wa habari kwamba shambulizi hilo huenda limechochewa na kauli za Rais Trump ambazo, alisema, ni za kibaguzi na chuki.

CNN iliripoti kwamba jumbe za chuki na ubaguzi zilizopatikana kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa zinachunguzwa kubaini kama ziliandikwa na mshukiwa huyo.

Idara ya upelelezi ya FBI ilitangaza Jumamosi usiku kwamba imefungua uchunguzi wa shambulizi hilo na utafanyika kwa misingi ya ugaidi wa ndani ya nchi.

Shambulizi la Jumamosi lilijiri chini ya wiki moja baada ya lingine, ambapo watu watatu, wakiwemo watoto wawili, kutokea kwenye tamasha la Chakula na Muziki mjini Gilroy, California.

El Paso ni mji ulio karibu na mpaka wa Marekani na Mexico na wakazi wengi ni wa asili ya Mexico.

XS
SM
MD
LG