Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 19:36

Waziri Mkuu Johnson alaani kauli za kibaguzi dhidi ya wachezaji Weusi


Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amelaani shambulizi la kibaguzi katika mitandao ya jamii dhidi ya wachezaji Weusi katika timu ya soka ya Uingereza baada ya kufungwa goli 3-2 na Italia kwenye mashindano ya Euro 2020 Jumapili.

Baada ya Italia na Uingereza kutoka sare 1-1 kufuatia muda wa nyongeza, timu hizo zililazimika kupiga penalti kutafuta mshindi.

Timu ya Italia ikisheherekea kuibuka kidedea katika mashindano ya Euro 2020.
Timu ya Italia ikisheherekea kuibuka kidedea katika mashindano ya Euro 2020.

Wachezaji weusi Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka walikosa penalti na kuwapa Italia ushindi.

Wakati maoni mengi katika mitandao ya kijamii yalikuwa chanya kwa timu ya Uingereza, wachezaji hao watatu walianza kupokea matamshi ya kibaguzi mara tu baada ya mchezo huo kumalizika.

Katika akaunti yake ya Twitter, Johnson amesema timu hiyo inastahili “kupongezwa kama mashujaa, na siyo kukejeliwa katika mitandao ya jamii.

Wale wanaohusika na udhalilishaji unaokera ni lazima waone haya.”

Kadhalika, Meya wa London Sadiq Khan, akituma ujumbe katika akauti yake ya Twitter, amesema hakuna nafasi ya ubaguzi katika michezo au sehemu yoyote nyingine. Amesema waliohusika lazima wawajibishwe.

Sadiq Khan
Sadiq Khan

Chama cha Mpira wa Miguu, Jumuiya inayosimamia soka Uingereza, walitoa tamko kulaani aina zote za ubaguzi na kuwaunga mkono wachezaji wake.

Idara ya polisi London imetuma ujumbe wa tweet kuwa ina taarifa za matamshi hayo ya kibaguzi, na kusema hayakubaliki na yatafanyiwa uchunguzi.

Wachezaji wa Uingereza wameonyesha msimamo thabiti dhidi ya ubaguzi wakati wa mashindano hayo, na kupiga goti kabla ya michezo yao ikiwemo fainali ya Jumapili.

Siyo mashabiki wote waliunga mkono ishara hiyo ya kulaani ubaguzi, na baadhi yao walikuwa wakizomea kupiga kwao goti.

Wakati Waziri Mkuu Johnson aliwasihi mashabiki kutowazomea wachezaji, baadhi ya wakosoaji wanafikiri kauli yake haikuwa ya kishindo, na hivyo ilikuwa inashajiisha ubaguzi.

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Sky News Jumatatu, mchezaji wa zamani wa soka Gary Neville alielekeza lawama kwa hatua aliyochukuwa Johnson.

Neville amesema, “Waziri Mkuu alisema kuwa ni sawa kwa watu wa nchi hii kuzomea wachezaji hao ambao walikuwa wanajaribu kuhamasisha usawa na kujihami dhidi ya ubaguzi.

Inaanza na wale walioko katika nafasi za juu za uongozi. Na hivyo mimi, sikushangazwa hata kidogo kuamka asubuhi ya leo na kukutana na vichwa hivyo vya habari.”

Vyanzo vya habari : Associated Press, Reuters and AFP.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG