Umoja wa Mataifa unatarajia hali kuwa mbaya, ukisema hauna rasilimali za kupambana na milipuko, na kadri inavyochukua muda mrefu kuanza kuambana nao, ndivyo hali itakavyozidi kuwa mbaya.
Kati ya Shirika la Afya Duniani na shirika la kuhudumia watoto UNICEF, Umoja wa Mataifa unatafuta dola milioni 640 za kukabiliana na ugonjwa huo wa kuambukiza, na kuonya kuhusu "janga la kipindupindu" kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
"WHO inakadiria kuwa watu bilioni moja katika nchi 43 wako katika hatari ya kupata kipindupindu," alisema Henry Gray, meneja wa matukio wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa la kukabiliana na kipindupindu duniani.
Hadi sasa mwaka huu, nchi 24 zimeripoti milipuko ya kipindupindu, ikilinganishwa na nchi 15 ilipofika katikati ya mwezi Mei mwaka jana.
Nchi ambazo kwa kawaida haziathiriwi na kipindupindu, sasa zimeathiriwa na idadi ya vifo imevuka ile ya kawaida ya kati ya watu 100.
Gray alilaumu ongezeko la visa hivyo linatokana na umaskini, migogoro na mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na watu kuhama makazi yao, ambayo huwaondoa watu kutoka katika vyanzo salama vya maji na chakula, na pia kuwa mbali na kwa msaada wa matibabu.
Kipindupindu huambukizwa kutokana na bakteria ambao kwa ujumla husambaa kupitia maji au chakula kichafu.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP.