Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 29, 2023 Local time: 11:15

Waraka wa Eid el Fitr : Serikali yashauriwa kuvumilia kusikia isiyoyapenda


Sheikh Ponda

Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Tanzania imetoa waraka wa salamu za Sikukuu ya Eid el-Fitr uliobeba ujumbe kuhusu haki na uhai; uhuru wa habari na kujieleza, wa Bunge na Mahakama, wa kisiasa na Katiba Mpya.

Waraka huo umeeleza siku za karibuni kulikuwapo na matukio mabaya yakiwamo ya kuokotwa kwa miili ya watu kwenye fukwe za bahari na mito hali inayoashiria haki ya kuishi imeanza kutoweka.

Waraka huo ulisomwa Jumamosi jioni na katibu wa jumuiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda katika Msikiti wa Mtambani uliopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.

“Jumuiya inaishauri Serikali ichukue hatua madhubuti za kurudisha amani ya wananchi na vyombo vya dola vinapaswa kulinda usalama wa wananchi. Ni wakati muafaka kwa tume ya kijaji kuchunguza masuala yote yanayohusu utekaji, kupotezwa na kuuawa watu,” alisema Ponda.

Uhuru wa habari, kujieleza

Vyanzo vya habari vimeripoti kuwa Sheikh Ponda alieleza haki na uhuru wa habari na kujieleza, vinaelekea kutoweka.

Alisema kanuni za maudhui zinazoongoza na kusimamia uendeshaji wa sekta ya habari nchini zinatumika zaidi kuuwa uhuru wa kupata habari na kujieleza kwa wananchi.

Alisema viongozi wa jumuiya hiyo wanaishauri Serikali iwe na uvumilivu wa kusikia hata mambo isioyapenda.

“Jamii ina haki na uhuru wa kutoa maoni juu ya namna Serikali yao inavyofanya kazi zake, maoni hayo yanaweza kutumiwa na Serikali katika kuboresha utoaji huduma wake,” alisema.

Sheikh Ponda alisema jamii ina uhuru wa kusoma, kuangalia na kusikiliza maoni hayo ya ukosoaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Alisema kupunguza uhuru wa watu kujieleza na kupata habari si njia nzuri ya kuongoza Taifa.

Uhuru wa Bunge na Mahakama

Alisema imeshuhudiwa kubanwa na kupungua kabisa kwa uhuru wa Bunge, kwanza kwa kufutwa kwa haki ya wananchi kuona matangazo ya moja kwa moja ya wawakilishi wao wakiwa bungeni kama ambavyo ilizoeleka..

Waraka huo wenye kurasa tisa umesainiwa na kaimu mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Sheikh Shaaban Hijja Mrisho na Ponda kwa niaba ya masheikh na maimamu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu.

Sheikh Ponda alisema waraka huo unatokana na kikao cha jukwaa kongwe la jumuiya hiyo lililokutana Juni 14 kujadili masuala mbalimbali ya kidini na ya kijamii.

Waraka wa TEC

Huo ni waraka wa tatu kutolewa na taasisi za dini, ukitanguliwa na uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Baraza hilo Februari lilitoa ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2018 ambao ndani yake ulieleza msimamo wa maaskofu 35 na mbali ya masuala ya kiroho, pia yalihusu ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Waraka wa KKKT

Machi 24, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), lilitoa waraka wa Pasaka ambao mbali ya masuala ya kiroho, ulitaja changamoto tatu na kuzifikisha kwa waumini.

Changamoto zilizotajwa katika waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa, na masuala mtambuka likiwamo suala la Katiba Mpya.

XS
SM
MD
LG