Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 01, 2022 Local time: 16:20

Kanisa la KKKT Tanzania: Waraka ulikuwa ujumbe ili serikali itafakari


Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mkuu wa Kanisa la KKKT Dkt Fredrick Shoo.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dkt Fredrick Shoo, amesisitiza waraka uliotolewa na maaskofu wa kanisa hilo haukuwa na nia mbaya na wala kanisa halikukurupuka kuuandika.

Askofu huyo alitoa ufafanuzi Jumapili mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, katika Ibada maalum ya uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi ya Kati ya kanisa hilo mjini Tabora.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe amesema kuwa kanisa hilo linaunga mkono jitihada zote zinazofanywa na Rais John Magufuli katika kuwaletea maendeleo wananchi na halina ugomvi na kiongozi yeyote katika serikali.

“Waraka uliotolewa na kanisa sio wa kukurupuka na haukutolewa kwa lengo baya dhidi ya serikali yetu kama baadhi ya watu wanavyopotosha,” alisema nakumwomba kila mpenda amani na maendeleo ya nchi hii aelewe hivyo.

Kauli ya Askofu Shoo

Kwa mujibu wa Askofu Shoo, lengo la waraka huo lilikuwa ni njia tu ya kufikisha ujumbe wa kanisa kwa serikali ili waweze kuutafakari na kufanyia kazi.

Hata hivyo, alisema kama kuna sehemu walieleweka vibaya, wako tayari kuomba radhi kwa nia njema ili kudumisha ushirikiano mzuri na serikali.

“Namshukuru sana Rais wetu, Dk. John Pombe Magufuli, kwa kuelewa dhamira yetu, ila wapo baadhi ya watu ndani ya kanisa na nje ya kanisa wasio na nia njema, wanaotaka kuchonganisha kanisa na serikali, watu wa namna hiyo wasifumbiwe macho, wana ajenda binafsi,” alisema.

Mwaliko wa Rais

Alimshukuru Rais kwa kukubali mwaliko wao na kumtuma Makamu wake, ili kujumuika nao katika ibada hiyo maalum ya Uzinduzi wa Dayosisi ya Magharibi ya Kati na kumsimika Askofu wa Dayosisi hiyo, Dk. Isaac Kissiri na Msaidizi wake, Mchungaji Newton John Maganga na kumuomba Samia awafikishie shukrani za kanisa kwa Rais.

Akitoa salamu za serikali, Samia alimpongeza mkuu wa kanisa hilo na maaskofu wote kwa kuanzisha dayosisi hiyo na kumsimika askofu mpya ili kupanua huduma za kiroho katika kanda hiyo.

Alisema serikali itaendele kushirikiana na madhehebu yote ya dini nchini na wapo tayari kupokea ushauri wowote kutoka kwa viongozi wa kiroho, ikiwamo kukoselewa.

Nasaha za Makamu wa Rais

Samia alisema serikali haina ugomvi na dhehebu lolote lile na ipo tayari kukosolewa, ila kinachotakiwa ni kufuata utaratibu mzuri wa kukosoa au kushauri badala ya kutumia lugha zisizofaa.

“Endeleeni kuwaombea wanasiasa wote na serikali yenu, tukosoeni pale tunapokosea, lakini tumieni lugha zinazokubalika ili tuelewane,” alisema.

Aliwataka maaskofu na wachungaji wote kuendelea kuhubiri amani na utulivu na kuonya kuwa serikali haitasita kumchukulia hatua mtu yeyote mwenye nia ovu anayechochea uvunjifu wa amani nchini.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG