Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 18, 2024 Local time: 05:25

Chenge asema kitendo cha polisi ni cha ovyo, kinyama


Mbunge Joshua Nassari
Mbunge Joshua Nassari

Mkazi wa Kitongoji cha Kiswanya, Mkoa wa Morogoro nchini Tanzania Amina Mapunda (26), alijifungua nje ya kituo cha polisi baada ya kutolewa mahabusu alikokuwa akishikiliwa kwa tuhuma zilizomhusu mumewe anayedaiwa kununua kitanda cha wizi.

Baada ya watu walioibiwa kutoa taarifa, polisi walichukua jukumu la kwenda kupekua katika nyumba ambayo ilisemekana ina vifaa vya wizi, lakini muhusika ambaye ni mume wa mama huyo (Abdallah Mohamed) hakuwapo nyumbani, vyanzo vya habari vimeripoti.

Gazeti la Nipashe limeripoti kuwa mwanamke huyo aliyelazwa Kituo cha Afya Mang'ula alikopelekwa kulazwa baada ya kujifungua, alikamatwa Juni 1, 2018 baada ya polisi, mwenyekiti wa kitongoji na mgambo, waliokuwa wakimtafuta mumewe kwa tuhuma za ununuzi wa kitanda cha wizi.

Mwanamke huyo alidai kuwa akiwa mahabusu, licha ya kulalamika kuumwa uchungu, askari wa zamu alimpuuza hadi alipoona amezidiwa na kumtoa nje na alijifungua kwenye nyasi bila msaada.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni, alitoa kauli ya serikali bungeni Ijumaa baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, kumtaka kufanya hivyo.

Kabla ya kumtaka naibu waziri huyo kutoa kauli ya serikali, kiongozi huyo alisema tukio hilo ni la ovyo na la kinyama akiwaunga mkono wabunge walioonyesha kukerwa na kuomba mwongozo kwa Kiti cha Spika.

Licha ya mwongozo kuhusu jambo hilo ulioombwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kutokidhi matakwa ya kikanuni, Chenge alisema tukio hilo ni baya na serikali inapaswa kulitolea maelezo.

Akitolea ufafanuzi kashfa hiyo bungeni, Masauni alisema suala hilo limeshafunguliwa jalada la uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa kwa watakaobainika.

"Naomba kutolea ufafanuzi kuhusu suala hilo. Serikali tunatoa masikitiko makubwa kuhusiana na tukio hilo lilivyojitokeza na tayari tumeshafungua jalada la uchunguzi," alisema.

"Kilichotufanya tulichukulie suala hilo kiundani ni kutokana na namna lilivyotokea. Tumelichukua kwa uzito wa hali ya juu, hivyo tutachunguza na uchunguzi huo ukikamilika hatua kali za kisheria zitachukuliwa."

Masauni alisema kilichoifanya wizara kulichukulia tukio hilo kwa undani ni kwa sababu kulikuwa na tukio la wizi lililomhusisha mume wa mwanamke huyo ambaye inadaiwa alinunua kitanda cha wizi.

Naibu waziri huyo alisema polisi walimtaka mama huyo aende polisi kwa ajili ya kusaidia polisi kwa sababu sehemu ya mali zilizoibiwa zilikuwa kwenye nyumba yake.

"Lakini hakufanya hilo, hivyo polisi wakachukua maamuzi ya kumchukua mwanamke huyo kwa lengo la kumhoji, kitu ambacho hakikuwa sahihi," alisema.

"Katika mazingira ya kawaida busara ingeweza kufanyika kwa sababu mama huyo alikuwa mjamzito. Wangeweza kumhoji akarudi nyumbani ndiyo maana tukasema tumelichukua kwa uzito na tunalichunguza."

XS
SM
MD
LG