Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Aprili 15, 2024 Local time: 00:03

Wakazi wa Kibiti, Mkuranga wamtaka IGP Sirro akutane nao


IGP Simon Sirro
IGP Simon Sirro

Wakazi wa wilaya za Kibiti na Mkuranga Mkoa wa Pwani nchini Tanzania wamesema iwapo mkakati wa Mkuu wa Jeshi la Polisi ( IGP ) Simon Sirro ni kukomesha mauaji aanze na mazungumzo.

Wamesema kuwa kwa kufanya mazungumzo na wananchi atabaini sababu zilizopelekea mauaji hayo na wahusika wanaoendesha mauaji hayo na suluhisho lake.

Mkazi wa Kibiti aliyejitambulisha kwa jina la Alhaji Msumi alisema IGP Sirro anapaswa kufika katika wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga kisha kufanya mazungumzo na wazee katika vijiji vya Bungu, Kibiti na Ikwiriri.

Mzee mwingine wa Ikwiriri ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema uzoefu wa Sirro katika utulizaji na utatuzi wa matatizo utafanikisha kuwabaini watu au kikundi wanaoendesha mauaji katika wilaya hizo.

“Tunafahamu uzoefu alionao IGP Sirro, hivyo tunaimani suala la mauaji atalikomesha mara moja,” alisema.

Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania limerepoti hayo na kuongeza kuwa mkazi huyo amesema kwa muda mrefu polisi walikuwa wakijua wilaya hizo hazipo salama kutokana na kukumbwa na matukio ya mauaji mara kwa mara, lakini walikuwa wazito kuanza kuusaka mtandao huo.

Amesema harakati za kuwasaka watu hao zimeanza pale yalipotokea mauaji ya aliyekuwa Ofisa Upelelezi Wilaya ya Kibiti, Peter Kubezya na wengine wawili ndipo walipoanza kuchukua hatua huku wakiwa wamechelewa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibiti, Gullamuhussein Kifu amesema hali ya usalama inazidi kuimarika siku baada ya siku na kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwakamata watuhumiwa wote.

XS
SM
MD
LG