Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Juni 19, 2024 Local time: 20:01

Wabunge wa CCM wataka waliohusika na mikataba mibovu wanyongwe


Bunge la Tanzania
Bunge la Tanzania

Serikali imetakiwa kufanya maamuzi magumu na kutoa adhabu ya kifo kwa watendaji wote wa serikali, waliohusika na mikataba mibovu, iliyosababishia taifa kuibiwa makinikia kwa muda mrefu.

Aidha serikali imeshinikizwa kuwasilisha bungeni mikataba yote ili iweze kupitiwa tena na itakayokutwa na makosa irekebishwe mara moja, kwa lengo la kuhakikisha Watanzania wanakuwa salama na rasilimali zao.

Mbunge wa Nkasi kwa tiketi ya CCM, Ally Keissy, ndiye aliyeibua hoja ya watendaji hao kunyongwa wakati akichangia kwenye mjadala wa Kamati ya Matumizi ya Bunge ya kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Keissy ametoa rai kuwa wakati umefika kufukua makaburi, kwa kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na mikataba mibovu.

Akiunga mkono hoja hiyo mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel (CCM) pia aliishauri serikali kuwasilisha mikataba yote bungeni, ili iweze kupitiwa kuondoa mapungufu.

“Nakubaliana na hoja ya Kessy kwamba kwa sasa Tanzania tunahitaji mikataba yote kupitiwa upya, na nina matumaini kuwa kwa hili tutafanikiwa kwani tayari rais ameonyesha dira,” alisema.

Naye mbunge wa Bukene, Selemani Zedi (CCM), alisema pamoja na kuiunga mkono hoja ya Keissy ni wakati muafaka sasa wa Bunge hilo kuanza kuipitia mikataba yote kutokana na ukweli kuwa bado mikataba mingi, ina maeneo yanayohitaji kurekebishwa kwa manufaa ya Watanzania.

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), alisema :“Mimi namuunga mkono Keissy katika hili, tufanye maamuzi magumu hata kama wahusika wasiponyongwa, lakini wachukuliwe hatua kali, pia na hii mikataba iletwe bungeni tuijadili na kupitia.”

Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema pamoja na kwamba waliohusika wameliingiza taifa katika hasara kubwa, kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba, zipo hatua kali za kisheria wanazoweza kuchukuliwa.

Hata hivyo, alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, zipo taratibu zilizotafsiriwa kisheria zinazoelezea makosa yanayosababisha mkosaji kunyongwa. “Makosa haya ya kupoteza rasilimali zetu pia yanaweza kutafutiwa adhabu kali kwa mfano kwa sasa tuna mahakama ya ufisadi. Lakini hili la kunyongwa lazima tufuate sheria zinavyosema,” alisema.

XS
SM
MD
LG