Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 15, 2024 Local time: 06:56

'Magufuli hajaamrisha Wakenya kufukuzwa Tanzania'


Rais Uhuru Kenyatta akicheka na mwenzake John Magufuli Ikulu ya Nairobi
Rais Uhuru Kenyatta akicheka na mwenzake John Magufuli Ikulu ya Nairobi

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania, imekanusha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii Kenya, kuwa Rais John Magufuli aliamrisha Wakenya kufukuzwa Namanga.

Vyombo hivyo vya habari, vimedai kuwa amri hiyo iliotolewa na rais ndio ilisababisha vurugu kati ya Watanzania na Wakenya ambayo iliendelea kwa siku mbili katika mpaka wa Namanga.

“Wizara inapenda kuwafahamisha kuwa habari hizo ni za uongo na zinakusudia kuchafua sifa ya Rais Magufuli ambayo amejitengenezea kwa kipindi chote na sura nzuri ya Tanzania kwa ujumla,” taarifa ya wizara imeeleza.

“Rais hajawahi kutoa amri kama hiyo kuhusiana na suala hilo la mpakani,” taarifa hiyo imeongeza.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara, Dr Aziz Mlima, Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia idara yake ya uhamiaji iliendesha zoezi la kawaida kuwaondoa wananchi wa kigeni wakiwemo Wakenya ambao wanaishi Tanzania bila ya vibali vya kazi au ukazi.

Katika taarifa hiyo katibu mkuu ameiomba serikali ya Kenya kupuuzilia mbali habari hizi za uongo na badala yake nchi hizi mbili ziendelee kuimarisha mahusiano mazuri ambayo tayari yapo kati yao.

Taarifa hiyo pia imehimiza vyombo vya habari na vyombo vya kijamii ikiwemo Televisheni ya taifa ya Kenya, NTV kuacha kueneza habari za uongo ambazo zinaweza kuleta usumbufu kwa wananchi wa nchi hizi mbili.

“Serikali ya Tanzania iko inayo nia ya kushirikiana na serikali ya Kenya katika nyanja zote ikiwemo miradi ya pamoja katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa maslahi ya wananchi wote,” imesema taarifa hiyo.

XS
SM
MD
LG