Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Februari 05, 2023 Local time: 16:29

Waislam Uganda wafanya maombi maalum dhidi ya dhulma, mauaji na utekaji nyara


Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislam wa Uganda

Maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu nchini Uganda wameshiriki maombi ya kitaifa kote nchini kutokana na ongezeko la mauaji, utekaji nyara na dhuluma za vyombo vya usalama na kutoweka kwa watu katika mazingira tatanishi.

Ibada kuu imefanyika katika msikiti mkuu wa Old Kampala, ikiongozwa na Mufti Shaban Ramadhan Mubaje. Maombi kama hayo pia yamefanyika katika kila msikiti kote Uganda.

“Tunawaombea wale wote waliouwawa, wanaozuiliwa gerezani kisiasa, hasa wanaozuiliwa kwa makosa ambayo hawakufanya, wanaopata vitisho dhidi ya maisha yao na taifa lote kwa ujumla,” amesema Kiongozi wa dini ya Kiislamu Uganda, Mufti Mubaje akiongezea kwamba maombi ya Ijumaa ni ya kidini na hayahusiani kwa namna yoyote na siasa za nchi hiyo.

Mufti Mubaje amesema kwamba ametembelea magereza mbali mbali na kugundua kwamba idadi kubwa ya wafungwa ni vijana walio katika umri wa miaka 20, wanaozuiliwa kwa sababu za kisiasa.

Kadhalika amesema kwamba maombi yataendelea kwa ajili ya kutaka haki kwa wanaozuiliwa gerezani, waliodhulumiwa na vyombo vya usalama, pamoja na waliouwawa.

Ongezeko la mauaji

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari mauaji yanayo walenga watu mashuhuri wakiwemo maafisa wa ngazi ya juu wa polisi, wanasiasa, na viongozi wa dini ya Kiislamu, yamekuwa yakitokea nchini Uganda, bila ya wahusika kukamatwa.

Washukiwa wa makosa mbalimbali wanadai kupigwa na kuumizwa na vyombo vya usalama wakati wanapo kamatwa au wakiwa kizuizini.

Maombi ya Waislamu yanajiri huku serikali ya Uganda ikiwa inashutumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wanasiasa wa upinzani.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG