Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Tunisia Mohamed Ben Zekri alisema wavuvi waligundua miili hiyo nje ya pwani ya mji wa Sfax.
Alisema abiria watano waliokolewa na wengine takriban 20 hawajulikani waliko.
Boti hiyo ilikuwa inavuka bahari ya Mediterranean kuelekea katika kisiwa cha Italia cha Lampedusa wakati ilipozama.
Msemaji wa Ulinzi wa Taifa Ali Ayari alisema boti hiyo ilikuwa imejaa watu na hali mbaya wakati ikikabiliana na upepo mkali, moja ya sababu ambazo anasema huenda zilichangia boti hiyo kuzama.
Kikosi cha jeshi la majini la Tunisia kinaendelea kuwatafuta waliosalimika, maafisa wamesema.
Ukiongezea matukio ya pwani ya nchi jirani ya Libya, ukanda wa pwani karibu na Sfax umekuwa mahali maarufu pakuanzia safari kwa watu wanaokimbia umaskini na vita Afrika na Mashariki ya Kati wakitafuta maisha bora Ulaya.
Idadi ya Watunisia wanaohangaika na matatizo ya kiuchumi inaongezeka katika nchi yao ambao pia wanakimbia pamoja na kuwepo juhudi za Rome kujaribu kuwashawishi kusitisha safari za kuvuka Mediterranean.
Wengi wa wahamiaji waliowasili Italia mwaka huu ni Watunisia.
Kati ya zaidi ya wahamiaji 34,000 waliowasili Italia mwaka huu, zaidi ya 12,800, au asilimia 38, ni raia wa Tunisia. Raia wa Bangladeshi ni kundi kubwa zaidi la pili, likifuatiwa na wahamiaji kutoka Ivory Coast, Algeria, Pakistan na Misri.