Mawaziri wakuu wa Ugiriki, Italy, Malta na Spain wameuandikia umoja huo barua wakisema kwamba mkataba huo hawueleweki na hauna mwelekeo maalum.
Vyanzo vya habari za kidiplomasia vimeliambia shirika la habari la AFP kwamba barua ya mawaziri hao wakuu imepelekwa kwa mkuu wa tume ya umoja wa ulaya Ursula von der Leyen, mkuu wa baraza la umoja huo Charles Michel na Kansela wa ujerumani Angela Merkel, ambaye nchi yake inashikilia kiti cha urais wa umoja huo.
Waziri mkuu wa uhispania Pedro Sanchez na waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte, ambao nchi zao za kusini mwa ulaya zinakabiliwa na mzigo wa kuwapokea wakimbizi, wametaja mkataba wa tume ya umoja wa ulaya kuhusu uhamiaji kuwa hautoshi.
"Tumepokea habari kutoka kwa umoja wa ulaya kuhusu mpango huo wa uhamiaji lakini tunasema kwamba hautoshi kwa sababu maswala kama mshikamano na sio tu uwajibikaji, bali mshikamano yanastahili kueleweka kabisa zaidi ya vile tume imependekeza.” Amesema Pedro Sanchez
Viongozi wataka ushirikiano zaidi kushughulikia wahamiaji
Tangu mgogoro wa uhamiaji ulipoanza mwaka 2015 na kupelekea zaidi ya wahamiaji milioni moja kuingia Ulaya, Sheria za umoja wa ulaya kuhusu uhamiaji zimetajwa kuwa na mapungufu mengi.
Japo serikali za nchi hizo nne hazina uwezo wa kufanya mabadiliko kuhusu sheria za uhamiaji za umoja wa ulaya, zimesema kwamba uhamiaji wa lazima unastahili kusalia kama chombo muhimu cha umoja.
Waziri mkuu wa Italia Giuseppe Conte, amesema kwamba wanataka kuhakikisha kwamba kuna mfumo wa uwajibikaji unaoambatana na mshikamano.
"Na tunahitaji kufanya kazi kuhakikisha kwamba kuna mfumo unaofaa katika ngazi ya umoja wa ulaya kwa sababu haiwezi kuwa kwamba nchi ambayo wakimbizi wanaingilia ndio inabeba mzigo wote.” Amesema Giuseppe Conte
Waziri mkuu wa Spain Pedro Samchez amesisitiza kwamba usalama kwenye mipaka ya Italia na spain inatosha.
Amesema kwamba "hilo sio tatizo. Tatizo ni namna tunavyowashughulikia watu hawa wanaowasili baada ya kusafirishwa na makundi ya uhalifu na kuwaweka katika hatari kubwa ya kufa mfano katika Atlantic wanapojaribu kufikia Visiwa vya Canary.”
Nchi nne zilizosaini makubaliano zipo kwenye mpaka wa umoja wa ulaya na wahamiaji hufikia kwanza mipaka yao.
Tume ya umoja wa ulaya inataka mabadiliko makubwa kwenye sheria za uhamiaji zinazotumika na nchi wanachama 27 ili mzigo wa kuwapokea wahamiaji unagawa kwa nchi zote za umoja huo na wala sio kuwachiwa Ugiriki, Italy, Malta na Spain.
Juhudi za kuwakagua wahamiaji zitaimarishwa mpakani kuwazuia wahamiaji wakiuchumi kuingia umoja huo, na kurudishwa nchi wanazotoka.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC