Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Agosti 14, 2022 Local time: 22:48

Uhuru aadhimisha Kumbukumbu ya Kenyatta kwa kuhimiza mshikamano


Rais Uhuru Kenyatta

Rais Uhuru Kenyatta ameeleza tofauti za kisiasa kuwa ni msingi wa demokrasia ya Kenya, lakini ameonya kuwa kuhitilafiana katika maoni kusitumike kugawa nchi.

Kenyatta, hata hivyo, alisisitiza kuwa tofauti hizo, ambazo amesema zilikuwa kubwa zaidi wakati wa uchaguzi lazima ziheshimiwe, kwani zinamafungamano ya moja kwa moja na maendeleo ya nchi.

“Hakuna hata Mkenya moja ambaye alikwenda kupiga kura katika uchaguzi huu na kufanya makosa (kwa kumpigia kura mgombea wa chaguo lao),” Rais Kenyatta amewaambia waliokusanyika katika Kanisa la St Stephen liliopo katika barabara ya Jogoo wakati wa ibada ya kumbukumbu ya 39 ya muasisi wa taifa la Kenya Rais Jomo Kenyatta.

Aliendelea kusema: “ Huo ndio uhai na msingi wa demokrasia. Na bila ya kuheshimu kuwepo tofauti kati yetu, hata ajenda yetu ya maendeleo haiwezi kufanikiwa.

“Ni lazima tuwe tayari kuheshimu uwezo wetu wa kuwa na maoni yanayokinzana na maoni tofauti hayamaanishi kuwa ni uadui, bado sisi ni kitu kimoja.”

Rais Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi baada ya uchaguzi uliokuwa na wasiwasi mkubwa Agosti 8 ambapo hasimu wake wa kisiasa Raila Odinga amekataa matokeo na kufungua kesi katika Mahakama ya Juu.

Kuhusu baba yake ambaye alifariki Agosti 22, 1978 wakati Kenyatta mtoto alipokuwa miaka 16, rais amemuelezea baba yake kuwa ni mtu ambaye alikuwa na mapenzi makubwa na nchi ya Kenya.

“Hivi leo tunaadhimisha na kukumbuka maisha ya mtu ambaye pamoja na wenzake alijitolea maisha yake kwa kuhakikisha Kenya inapata uhuru na kwa miaka 17 aliongoza taifa kama baba (muasisi) wa taifa hili,” amesema Rais Kenyatta, ambaye alikuwa amefuatana na mkewe Margaret na mama yake Ngina Kenyatta.

Rais Kenyatta alikuwa na matumaini kuwa yeye pamoja na wenzake wa rika lake walikuwa wanaendeleza yale ambayo Mzee Kenyatta na mashujaa wa uhuru walikuwa wanapendelea yafanyika kwa ajili ya nchi yao.

“Sio kwamba hatujawahi kufanya makosa… Tumekuwa tukifanya makosa. Lakini tumeweza kujifunza kutokana na makosa yetu. Na nina uhakika kuwa wazee wetu watajivunia kwa mafanikio tuliyoweza kuyafikia,” amesema Rais Kenyatta

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG