Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Julai 22, 2024 Local time: 20:49

Tanzania yalaani ufukuaji makaburi ya wenye ulemavu wa ngozi


Ukatili dhidi ya albi
Ukatili dhidi ya albi

Mkutano ulioshirikisha wadau wa haki za binadamu umefanyika Alhamisi Dar es Salaam kuhusiana na haki za watanzania wenye ulemavu wa ngozi (Waalbino) ambapo sasa kuna tuhuma za ufukuaji wa makaburi yao.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa katika ofisi za tume ya haki za binadamu na utawala bora jijini DSM mkutano huu umewashirikisha wadau kutoka mahakama, taasisi za kiraia, ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali , na tume ya kurekebisha sheria.

Washiriki wote hawa wakiwa ni wadau muhimu katika mapambano ya kutafuta haki za watu wenye ulemavu wa ngozi.

Ameripoti kuwa wakati juhudi hizi zinafanyika kumekuwa na ripoti kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi makaburi yao sasa yanafukuliwa licha kuwepo mauaji, utekaji, na ukataji wa viungo vyao.

Mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu na utawala bora Bahame Nyanduga amesema kuwa tathmini iliyofanywa na tume inaonyesha kuwa tatizo hili limekuwepo tangu mwaka 2006, lakini linaonekana hivi sasa limejitokeza kwa nguvu.

"Napenda kuwashukuru kwa kuliibua tatizo hili kwani inaonekana watu hawa walinyimwa haki zao wakiwa hai na sasa wananyimwa haki zao hali ya kuwa wameshakufa.

Amezitaka Wizara ya Serikali za Mitaa chini ya ofisi ya Rais pamoja na halmashauri zake watizame jinsi ya kutenga mafungu katika bajeti kwa ajili ya kutoa elimu itakayo ondoa unyanyapaaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kutokomeza ukatili wanaofanyiwa.

Kwa upande wao wadau hao wa haki za binadamu walitaka kuwepo sheria kali zaidi kwa watakaokutwa na hatia katika kesi zinazohusisha watu wenye ulemavu wa ngozi.

Wametaka kuwa elimu ya haki za binadamu ianze kutolewa kuanzia ngazi za chini.

Mwakilishi wa shirika la kimataifa la utetezi wa watu wenye ulemavu wa ngozi la under the same sun, Vicky Mtetema ameomba kuwepo na takwimu sahihi za matukio yanayohusiana na ukatili wa watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwemo matukio ya hivi karibuni ya ufukuaji wa makaburi waliozikwa.

Mwandishi wetu ameripoti kuwa tangu kuanza kwa ukatili huu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini imeelezwa kwamba jumla ya kesi 65 za watuhumiwa wa mauaji na ukatili wa watu hao zimefikishwa kwenye vyombo mbalimbali vya Mahakama huku kesi saba zikiwa zimetolewa hukumu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Dina Chahali, Tanzania

XS
SM
MD
LG