Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Oktoba 01, 2023 Local time: 11:37

Kenya na Tanzania zamaliza mgogoro wa Namanga


Rais Magufuli na Rais Kenyatta

Wakenya wanaoishi karibu na mpaka wa Namanga wamepambana na polisi wakati wakiandamana kupinga kunyanyaswa na vyombo vya kisheria nchini Tanzania, ikizua mgogoro kati ya wakazi wanaoishi katika maeneo ya mpakani.

Hata hivyo viongozi wa eneo hilo waliingilia kati Jumatatu na kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Longido, Daniel Chongolo pande zote mbili Kenya na Tanzania zimefikia makubaliano kumaliza mgogoro huo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Kenya, Washington Oloo amesema yale yaliyoleta utata mpakani Namanga yametatuliwa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania wananchi wote wametakiwa kufuata sheria na hivyo wanaotaka kuishi Tanzania lazima wafuate taratibu sawa na watanzania wanaotaka kuishi upande wa Kenya.

Wananchi hao wa Kenya walichoma matairi katikati ya barabara wakizuia shughuli za usafiri na kutishia kuwafukuza wananchi wa Tanzania ambao wanaishi na kufanya kazi upande Kenya katika eneo la mpakani kama kubughudhiwa huko hakutakoma.

Maafisa wa polisi walitumia mabomu ya machozi kuwatawanya wakazi wenye hasira ambao walizuia magari yakiwa na namba za usajili za Tanzania kuingia Kenya.

Hali ya Taharuki ililikumba eneo la Namanga Jumatatu baada ya wananchi wa Kenya kufunga eneo huru la Nomad Land.

Wananchi hao wa Kenya walizuia magari yaliyokuwa yanatoka Tanzania kuingia Kenya wakishinikiza kuachiwa wenzao waliokamatwa kwa madai ya kuishi upande wa Tanzania bila kibali.

Wakenya hao pia waliharibu matenki ya maji ambayo yamekuwa yakisambaza maji upande wa Tanzania kutoka Kenya.

Kwa mujibu wa Uhuru Ole Sirote, Mjumbe wa Nyumba Kumi, wafanyakazi wa kwenye mabaa katika klabu za Kenya wameambiwa waondoke nchini Kenya kama ni njia ya kulipiza kisasi.

XS
SM
MD
LG