Uamuzi huu wa mahakama umekuja mara baada ya kiongozi mkuu wa Muungano wa Upinzani wa Nasa nchini Kenya kujiondoa katika kinyang’anyiro cha Urais ulioratibiwa Octoba 26.
Wakati huohuo bunge la kitaifa limeidhinisha mapendekezo ya kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi.
Kufuatia uamuzi huu wa Mahakama Kuu kumruhu Ekuru Aukot kuorodheshwa katika sajili ya wagombea Urais, mgogoro wa kisiasa na kikatiba unaonekana kujidhihirisha kuiweka nchi katika njiapanda.
Wachambuzi wa siasa na katiba nchini Kenya wanaeleza kuwa IEBC imejikuta katika hali ya utata na hivyo basi huenda ikahitajika kukimbilia mahakama ya Juu kutafuta ufafanuzi zaidi wa kisheria la sivyo watajikuta katika mzozo wa kikatiba ambao hujawahi kushuhudiwa nchini.
Imeonekana kuwa afueni kwa Ekuru Aukot na wafuasi wake baada ya mahakama kueleza kwa kina kuwa haki zake za kikatiba zilikuwa zimehujumiwa kufuatia uamuzi wa tume ya uchaguzi kumuondoa kwenye orodha ya wagombea wa Urais katika uchaguzi wa Oktoba.
Jaji John Mativo akisisitiza kuwa haipo sababu yoyote ya kumuondoa kiongozi huyo ambaye ni mtaalam wa katiba na sheria kwenye kinyang’anyiro cha Urais.
Hata hivyo, Aukot kando na kusisitiza kuwa IEBC ni sharti iondoe baadhi ya maafisa wanaosemekana kuhujumu kura ya Urais ya awali, anaeleza kuwa ataandaa mkutano wa kilele wa chama chake kuafikia masuala muhimu ambayo wataikabidhi IEBC kuyashughulikia kabla ya kuandaa uchaguzi mwingine.
Hatua hii inajiri wakati bunge la kitaifa nchini Kenya limeidhinisha kwa kauli moja mswada wa mapendekezo yanayopania kuzifanyia marekebisho sheria za uchaguzi.
Na hata japo mswada huo sasa umeelekea katika bunge la Seneti, bunge hilo limetupilia mbali pendekezo la kumtaka mwenyekiti wa tume ya uchaguzi asiwe mwanasheria, pendekezo la kumtaka Naibu mwenyekiti wa tume hiyo kuchukua majukumu ya Mwenyekiti iwapo atakosekana pamoja na idadi kamili ya kufanya maamuzi muhimu ya tume nzima.
Lakini Boby Mkangi Mtaalam wa Sheria na Katiba nchini Kenya anaeleza kuwa hatua hiyo ya wabunge wa chama cha Rais Uhuru Kenyatta huenda isiwe na uzito wowote katika uchaguzi wa mwaka huu iwapo utakuwepo.
Na kando na Mahakama ya Juu hivi leo kutangaza kuwa wiki ijayo Jumanne itatoa uamuzi kuhusu kesi ya Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati anayetaka ufafunuzi wa kumtangaza mshindi wa Urais,Wafuasi wa Odinga ambao wamekuwa wakiandamana leo katika miji mikuu nchini Kenya wanafurahia uamuzi wake wa kujiondoa katika kinyang’anyiro cha Urais hadi pale IEBC itimize masharti yake.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya