Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 28, 2023 Local time: 15:08

Trump atahadharisha juu ya ajenda ya kisoshalisti


Rais Donald Trump akihutubia mkutano mkuu wa Warepublikan Alhamisi Agosti. 27, 2020, Washington DC. (AP Photo/Alex Brandon)

Rais Donald Trump alirejea kauli mbiu yake Alhamisi usiku aliyoitoa katika hotuba ya mkutano mkuu wa chama hicho mwaka 2016 na siku ya kuapishwa kwake mwaka 2017.

Rais Trump alisema : “Uchaguzi huu utaamua iwapo tunaiokoa ndoto ya Marekani, au kama tutaruhusu ajenda za kisoshalisti kuvunja hatima yetu bora.”

Rais alihitimisha mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha Republican Alhamisi usiku kwa hotuba ya kukubali rasmi uteuzi wa chama chake mbele ya watu takriban 1,500 waliokuwepo kwenye eneo la South Lawn huko White House.

Kama ilivyokuwa kwa ndugu zake wakubwa ambao walizungumza mapema wiki hii, Ivanka Trump alihutubia mkutano huo wakati wa kumkaribisha baba yake.

Ivanka Trump ambaye ni mshauri wa rais alisema :“Leo usiku, nasimama mbele yenu kama mtoto mwenye kujivuna wa rais wa watu.”

Wakati nchi inaendelea kugubikwa katika ghasia za kijamii na maandamano ya mitaani, Trump alisisitiza kuhusu sheria na utaratibu, akijaribu kuelezea kuwa makamu rais wa zamani Joe Biden ni ‘farasi wa jeshi’ ambaye amedhibitiwa na watu wenye mtizamo wa mrengo wa kushoto katika chama cha Democratic.

Rais Trump alisema :“Joe Biden ni dhaifu. Anatekeleza amri kutoka kwa ndumila kuwili ambao wanaisukuma miji kuanguka wakati wakikimbia mbali kabisa na matukio ya uharibifu.”

Mikutano yote miwili mikuu ya Democratic na Republican imekosolewa kwa kulenga sana kuhusu tabia ya mtu, kumsifia mgombea na kumbeza mpinzani, na siyo kuzungumza vya kutosha kuhusu sera zao.

William Howell wa Chuo Kikuu cha Chicago amesema :“Hilo ni kweli kabisa nadhani katika mkutano mkuu wa RNC. Bado hatujaona picha ya wazi kuhusu masuala gani ambayo rais anataka kukabiliana nayo. Kuna ahadi zisizo wazi katika hilo, kwanza alizungumzia kuhusu uchumi mzuri, ataurejesha tena. Lakini hakuna maelezo yeyote jinsi atakavyofanya hivyo, au hatimaye jinsi atakavyoshughulikia janga hili.”

Chini ya theluthi moja ya Wamarekaani wanaidhinisha jinsi Trump anavyokabiliana na janga la Covid 19. Alijitetea mbele ya watu 1,500 ambapo wachache tu walikuwa wamevaa barakoa na kukaa karibu karibu. Wengi wao inadaiwa hawajapimwa kama wana Covid 19.

Hotuba ya Trump imehitimisha mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha Republican ambao ulivunja utamaduni ulizoeleke na taratibu, ikiwemo maamuzi ya kufanya baadhi ya matukio huko White House huku baadhi wakikosoa kuwa ni ukiukaji wa maadili, akichanganya kampeni na utawala.

Mkutano mkuu ulilenga zaidi maeneo ya wafuasi wa Trump, pamoja na makundi ambayo yalionyesha uungaji mkono mdogo kwake, yaani wanawake na watu walio wachache. Ikiwa ni pamoja na hotuba ya Alice Johnson, mwanamke mweusi ambaye hukumu yake ya kifungo cha maisha kwa shutuma za dawa za kulevya Trump aliifuta, na Ann Dorn mjane wa afisa mweusi mstaafu ambaye aliuawa wakati maandamano.

Amanda Iovino, Mrepublican anayeandaa mikakati alisema : “Umeonyesha ubinadamu kwa Alice Johnson, na kuleta mageuzi katika sheria ya uhalifu. Nadhani kilichotia hamasa kubwa katika hotuba ya usiku ni Ann Dorn. Kwa mara nyingine tunauona uso na kuweka hisia kwa sheria na utaratibu ambao mara kwa mara tunaweza kusikia sauti kali, lakini nadhani kwa kweli alichokieleza kimetufikisha nyumbani, na kubainisha umuhimu wa wapiga kura wa mijini.”

Wakati Trump akizungumza, waandamanaji walikuwa nje ya White House, ikiwa ni dalili kwamba nchi bado itabaki katika mtizamo mchanganyiko wakati ikielekea katika uchaguzi wa mwezi Novemba.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Harrison Kamau, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG