Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 02, 2024 Local time: 00:20

Vyombo vya dola vyaionya TLS Tanzania


Tundu Lissu
Tundu Lissu

Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), limeonywa kutoingilia vyombo vya uchunguzi na upelelezi, vinavyoshughulikia mlipuko uliotokea kwenye ofisi za Kampuni ya Mawakili ya IMMMA usiku wa kuamkia juzi jijini Dar es Salaam.

Baraza hilo nchini Tanzania limefahamishwa kuwa kama kutatokea wateja watakaolalamika kuwa mawakili wao hawakufika mahakamani siku ya Jumanne na Jumatano, hatua za kisheria dhidi ya mawakili hao zitachukuliwa, ikiwemo kuwapeleka kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili.

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma ameyasema hayo na kuongeza kuwa TLS hawana haki ya kutoa agizo kwa mawakili, kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza mengine, kwa kuwa kila wakili ana mkataba binafsi na mteja wake.

Onyo hilo limekuja baada ya Rais wa TLS, Tundu Lissu kuwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa Baraza lao la uongozi lina taarifa kuwa kikundi cha watu wenye silaha za moto, wakiwa wamevalia sare za Jeshi la Polisi, kiliwateka nyara walinzi binafsi wa Kampuni ya IMMMA na kuingia ndani ya eneo la ofisi hizo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari Tanzania Lissu alidai watu hao baada ya kuingia ndani kwenye ofisi hizo, walitega milipuko na madumu manne ya mafuta ya petroli katika maeneo kadhaa ya jengo la ofisi hizo. Alidai muda mfupi baadaye, milipuko hiyo ililipuka na kusababisha uharibifu mkubwa wa jengo la ofisi za IMMMA Advocates zilizoko Upanga pamoja na majengo jirani.

Profesa Juma amesema uhuru wa mahakama ni pamoja na kuheshimu mamlaka nyingine za nchi zinapokuwa zinafanya kazi zake. Alisema kwa kuwa tukio la kulipuliwa kwa ofisi za Mawakili wa Immma ni tukio la kihalifu, hivyo wanasheria waiache Polisi na vyombo vingine vya upelelezi kufanya kazi yao.

TLS hawana haki ya kutoa agizo kwa mawakili, kutohudhuria mahakamani na kwenye mabaraza mengine, kwa kuwa kila wakili ana mkataba binafsi na mteja wake, amesema Profesa.

Kwa upande wake Jeshi la Polisi limesema liachwe liendelee na kazi ya uchunguzi, badala ya kulihusisha na tukio hilo. Msemaji wa Jeshi hilo Makao Makuu, Kamishina Msaidizi Barnabas Mwakalukwa alisema Jeshi la Polisi ndicho chombo chenye mamlaka ya kufanya uchunguzi na hivyo kama kuna mtu yeyote mwenye taarifa yoyote kuhusu tukio hilo, anatakiwa kuzitoa polisi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari.

“Kama Lissu ana hizo taarifa alitakiwa azilete polisi kwa kuwa ndicho chombo cha uchunguzi badala ya kuzungumza na vyombo vya habari. Kazi ya polisi ni kufanya uchunguzi wa kina na ndiyo maana Kaimu Kamanda wa Kanda Maalumu alisema atatoa taarifa uchunguzi ukikamilika, hivyo watu wanapaswa kusubiri taarifa kamili, nje ya hapo tunakuwa tunafanya kazi nje ya utawala wa sheria,” alieleza Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mwakalukwa.

Mwakalukwa alivitaka vyombo vya habari, kuwatafuta walinzi hao ambao Lissu alidai walitekwa na watu wanaodhaniwa kuwa polisi ili waeleze tukio lilivyokuwa na ikibidi walinzi hao kutoa taarifa za kutekwa kwao polisi.

XS
SM
MD
LG