Waziri aliyasema hayo mwisho wa wiki bungeni na kueleza kuwa wakuu wa wilaya na mikoa wanapaswa kutumia busara katika kuwaweka watu ndani.
“Msiniponze. Mimi nataka Rais Magufuli asinibadili hapa, mimi nataka Rais Magufuli aseme mzee endelea, tuache masuala ya umwamba, nawaomba huko mliko msiniharibie kazi yangu. Mimi ndiye mwenye cheo cha utawala bora, mimi ndiye waziri mwenye dhamana ya utawala bora, ukiendesha mambo kinyume cha utawala bora unaniharibia kazi,” alisema Mkuchika.
Alisema madaraka ya wakuu wa wilaya kuwaweka ndani watu saa 24 ni kwa usalama wao washukiwa.
“Lugha iliyotumika ni kwa usalama wake, maana yake mtu ameua mtu na jamaa zake wamekasirika wanataka kumpiga yule aliyeuwa na hapo ndipo dhana ya kumweka huyo mtu ndani saa 24,” amefafanua.
Alisema mkuu wa wilaya baada ya saa 24 kumalizika, ikifika asubuhi ni lazima ampeleke mtuhumiwa mahakamani.
“Nataka niseme mahali popote mkuu wa wilaya kumweka ndani mtu saa 48 ni makosa kwa sababu sheria inampa saa 24 na mkuu wa mkoa amepewa saa 48,” amesisitiza Mkuchika.
Kwa upande wa wakuu wa mikoa wamepewa mamlaka ya saa 48 na akipenda anaweza kumweka mtuhumiwa ndani saa 24 na si lazima amweke mtu ndani.
“Kama ni kosa la jinai Mkuu wa Polisi wa Wilaya yuko. Kama ni suala la uhamiaji mtu wa uhamiaji yupo, kama amekwepa kodi mtu wa Mamlaka ya mapato Tanzania yupo, si lazima utamke wewe,” alisema Mkuchika.
Rais Magufuli, mwezi Januari 2019, akiwa kwenye hafla ya kuwaapisha majaji, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapya Ikulu jijini Dar es Salaam, aliwataka wakuu wa wilaya aliyowateua kwenda kusimamia sheria, kutoitumia vibaya sheria ya kuwaweka watu polisi.
“Tumefanya mabadiliko madogo kwenye wilaya mbili, wilaya ya Mwanga kila mtu amesikia, kuna wakati DAS aliwekwa ndani, mara mkurugenzi. Vurugu zote ukizifuatilia zinaanza na Mkuu wa Wilaya,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema wakuu wa wilaya wanasheria na mamlaka walizopewa lakini wasitumie vibaya mamlaka hayo.
“Viongozi wengi wamezungumza kuhusu hili na mimi narudia. Kama una mamlaka ya kuweka watu ndani sawa. Je, mkuu wako wa mkoa na yeye akiamua kuweka ndani, si itakuwa vurugu?
Kuna masuala mengine hayahitaji kuwekana ndani yanahitaji maelekezo, hapa pawe hivi, hivi,” alisema Rais Magufuli.
Alisema kitendo cha mkuu wa wilaya kumweka mtu mahabusu kisha kumtoa bila kumpeleka mahakamani si haki.