Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 25, 2024 Local time: 20:12

Tanzania : CUF - Maalim yatoboa siri ya mkutano wa CUF- Lipumba


Profesa Ibrahim Lipumba
Profesa Ibrahim Lipumba

Wanachama wanaomuunga mkono Kiongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif, umewatahadharisha wajumbe wanaomuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye anatambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutohudhuria mkutano ulioandaliwa kufanyika Machi 12 -15 kumuondoa kiongozi wao.

Wanachama hao wamewataka wajumbe kutoka nje ya Dar es Salaam kutohudhuria mkutano huo na kudai wako tayari kukilinda chama chao kwa gharama yoyote, limeripoti gazeti la Mtanzania Jumapili.

Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam, Jumamosi na Naibu Katibu Mkuu CUF-Maalim, Joran Bashange, katika ukumbi wa ofisi ya wabunge iliyopo Magomeni, ikiwa ni siku moja baada ya upande wa Lipumba kupitia Kaimu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya, kueleza kuwa bodi ya wadhamini wa CUF imepewa usajili na Wakala wa Usajili na Udhamini (Rita) baada ya kukidhi vigezo.

Bashange alisema Lipumba anayedaiwa kushirikiana na Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, amepanga kumfukuza uanachama Maalim Seif na viongozi wenzake halali.

Alisema wameshapata taarifa za njama ya uitishwaji wa mkutano mkuu wa taifa "feki" wa Lipumba na genge lake, lakini Mei 9, mwaka 2018 yeye pamoja na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Nassor Ahmed Mazrui, walifungua shauri mama namba 84/2018 na shauri dogo namba 248/2018 kupinga kuitisha mkutano huo feki.

“Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Magoiga, Februari 28, mwaka 2019 ilitoa hukumu baada ya kuhitimisha kusikiliza shauri dogo namba 248/2018 na kutoa amri ya zuio, ikimzuia Lipumba na genge lake, wakala wao au yeyote anayefanya kazi chini yao kuitisha mkutano mkuu wa taifa kwa jina la CUF hadi shauri la msingi namba 84/2018 litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” alisema.

Amefafanua kuwa hata hivyo kwa jeuri na majivuno Lipumba na "genge lake" wameazimia kupuuza amri ya mahakama na kuamua kuendelea na mkutano mkuu wao uliotangazwa kufanyika Machi 12 hadi 15 katika Ukumbi wa Lekam uliopo Buguruni Malapa, Ilala Dar es Salaam.

Bashange alisema kwa mujibu wa taarifa ya Jaffari Mneke kupitia vyombo vya habari Machi 6, mwaka 2019, tayari Msajili wa Vyama vya Siasa alikwishawapatia fedha takriban Sh bilioni moja.

“Taarifa kutoka vyanzo sahihi zinaonyesha kuwa wameshaanza maandalizi yote ikiwemo uchapishaji wa fulana, kuchoresha mabegi ya mkutano huo na kuhakikishiwa ulinzi wa polisi,” alisema Bashange.

Alisema CUF kwa kuheshimu sheria kimemwandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro na kupeleka nakala kwa Rais, Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, OCD Kituo cha Polisi Buguruni na jumuiya ya kimataifa kuwataarifu kusudio hilo la uvunjaji wa amri halali ya mahakama.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG