Mwanasiasa huyo mkongwe mwenye umri wa miaka 73, ambaye alichaguliwa kwa wingi wa kura za wabunge jana Jumatano, kuwa kiongozi wa nchi hiyo, alikula kiapo, huku mkuu wa polisi wa nchi hiyo na mkuu wa jeshi wakisimama nyuma yake.
Vyanzo rasmi vya habari vilisema kiongozi huyo mpya anatarajiwa kuunda baraza la mawaziri hivi karibuni litakalojumuisha wabunge kadhaa wa upinzani ili kuiondoa nchi hiyo katika mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi tangu kupata uhuru kutoka kwa Uingereza.
Kiongozi wa upinzani Sajith Premadasa, ambaye alimuunga mkono mgombeaji mpinzani katika kura hiyo ya Jumatano, alisema amekutana na Wickremesinghe kujadili jinsi ya kulinda nchi hiyo dhidi ya "mateso na matatizo" zaidi.
"Sisi kama upinzani tutatoa msaada wetu mahsusi, kwa juhudi za kupunguza mateso ya wanadamu," Premadasa aliandika kwneye ukurasa wake wa twitter leo Alhamisi.
Wikremesinghe amewahi kuhudumu kama waziri mkuu kwa mihula sita.