Katika barua kwa rais Museveni, Kadaaga amesema kwamba kinyume na taarifa za maafisa wa serikali kwamba mbunge Bobi Wine hakupigwa, mbunge huyo ana alama zinazo onekana wazi za kupigwa na kuumizwa.
“Rais, ninalazimika kukuandikia kufuatia vitendo vya maafisa wa usalama kuwapiga wabunge, raia na waandishi wa habari. Maafisa wa kikosi chako cha ulinzi SFC, wanajeshi na maafisa wa polisi walihusika na hadi sasa, hakuna hatua imechukuliwa kuwakamata. Hatua yao ilivunja sheria dhidi ya dhuluma, ya mwaka 2012, ibara ya 2, 1(a) na (b),” ameandika spika Kadaaga.
Spika Kadaaga amemweleza Museveni kwamba iwapo maafisa hao hawatakamatwa, basi itakuwa vigumu kwake kusimamia shughuli za bunge.
Wakati huo huo, msemaji wa jeshi la Uganda (UPDF) Brig Richard Karemire, amesema kwamba jeshi halina kesi yoyote dhidi ya Bobi Wine, bila kueleza nani alikuwa mmiliki wa bunduki mbili, risasi kadhaa na madawa ya kulevya, vitu vilivyopelekea Bobi Wine kufikishwa katika mahakama ya kijeshi.
Polisi wa Uganda walionyesha waandishi wa habari bunduki, risasi na mikebe ya rangi nyeupe iliyoripotiwa kuwa na dawa za kulenya, na kusema kwamba vitu hivyo vilipatikana katika chumba chake Bobi Wine katika hoteli mjini Arua baada ya msako wa siku mbili kufuatia machafuko siku ya mwisho ya kampeni katika uchaguzi mdogo.
Jeshi lilimfunguliwa mashtaka ya uhaini kwa kupatikana na silaha hizo lakini baadaye mashitaka hayo yakafutiliwa mbali na mahakama ya kijeshi.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennes Bwire, VOA, Washington DC