Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Februari 06, 2023 Local time: 00:23

Pyongyang yaahirisha jaribio la nyuklia ikiepusha mvutano na Marekani


Maandamano ya kusherehekea siku ya jua Korea Kaskazini

Korea Kaskazini haikuendelea na azma yake ya kufanikisha jaribio la nyuklia Jumamosi, baada ya Marekani kuonyesha uwezekano wa kweli wa kutumia nguvu za kijeshi katika eneo hilo na China kuongeza shinikizo la vikwazo vya uchumi dhidi ya mshirika wake ambaye anamtegemea kiuchumi.

Badala yake kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un aliongoza gwaride la kijeshi katika kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa muasisi kiongozi wa nchi hiyo hayati Kim II Sung inayosheherekewa April 15, ambayo ni sikukuu muhimu sana kwa nchi hiyo inayojulikana kama siku ya jua.

“Kim Jong Un alikuwa amepanga kupambana na Marekani, lakini akaamua kuachilia mbali mpango huo,” amesema mkimbizi wa Korea Kaskazini na mchambuzi Ahn Chan-il ambaye yuko na Taasisi ya World Institute inayofanya tafiti juu ya Korea Kaskazini.

​Shinikizo la Kijeshi

Matarajio ya majaribio ya nyuklia yaliokuwa yamesambaa yaliongezeka wiki hii kutokana na taarifa za matukio ya hivi karibuni katika kituo cha majaribio ya nyuklia cha Punggye-ri na utaratibu wa Pyongyang wa kufanya majaribio ya kiuchokozi ya kijeshi yaliokuwa yafanyike wakati mmoja na maadhimisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwa muasisi kiongozi wa nchi hiyo.

Kuanzia Januari 2016, Pyongyang imekuwa ikifanya majaribio hayo bila ya kujizuilia hata kidogo, ikifanya majaribio mawili ya nyuklia na kujaribu kutupa makombora ya ballistikali mbalimbali ya masafa ya kati na masafa marefu.

Mwaka huu Kim Jong Un ameeleza kuwa taifa lake liko katika hatua za mwisho za kumaliza kutengeneza kombora la ballistiki lenye uwezo wa kufika mabara mbali mbali (ICBM) ambalo pia linauwezo wa kuipiga nchi ya Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump hata hivyo ameweka kipaumbele cha juu katika hatua yakuizuia Korea Kaskazini kuweza kutengeneza kombora lenye uwezo wa kubeba bomu la nyuklia la masafa marefu la uhakika ambalo linaweza kutishia usalama wa taifa la Marekani.

Kikosi cha Marekani cha Pacific Command wiki hii kilituma manuari yake aina ya USS Carl Vinson yenye ndege zenye kubeba silaha za nyuklia za jeshi la majini, ambayo imebeba pia makombora ya vita na vikosi vya wanaanga vilivyoelekea katika eneo hilo.

Na wiki iliopita mashambulizi ya angani yaliofanywa na Marekani dhidi ya Syria kwa kutumia kwake silaha za kemikali yaliongeza uzito wa kauli ya uongozi wa Trump kwamba pia iko tayari kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini.

Kufuatia shambulizi nchini Syria, Shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA limesema kuwauongozi wa Trump, “ umeingia katika njia ya kuanzisha vitisho na ufisadi.”

Sitisho la muda

Wakati ikionyesha kama vile Pyongyang imerudi nyuma kutokana na presha ya kijeshi iliyowekwa na Marekani hivi sasa, inawezekana ikawa ni sitisho la muda mfupi.

Manuari yenye kubeba makombora ya ballistiki inayotembea ndani ya maji ikionyeshwa kwenye sherehe za Korea Kaskazini
Manuari yenye kubeba makombora ya ballistiki inayotembea ndani ya maji ikionyeshwa kwenye sherehe za Korea Kaskazini

​Gwaride la kijeshi lililofanyika Jumamosi lilionyesha kwa ufahari manuari zenye makombora ya ballistikali (SLBM) inayosafiri ndani ya maji kwa mara ya kwanza, wakionyesha kuwa wamepiga hatua na kupanua uwezo wao wa kijeshi.

Choe Ryong Hae, msaidizi wa karibu wa Kim alilihutubia uwanja uliokuwa umefurika watu na akaendelea kuionya Marekani.

“Kama Marekani itaanzisha uchokozi wa kijinga dhidi yetu, nguvu zetu za kimapinduzi zitapambana naye mara moja na shambulizi la maangamivu, na tutajibu na vita kamili na itakuwa vita ya nyuklia na kwa mtindo wetu wenyewe wa kutumia silaha za nyuklia katika vita hiyo,” amesema.

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini mapema viliionya Marekani kusitisha “hamasa za kijeshi” lasivyo, “nguvu zetu za kukabiliana na Marekani na manuari zake zitatumika bila ya huruma kwa kuhakikisha kuwa wavamizi hawa wanaagamia.”

Shinikizo la kiuchumi

Trump pia ameishinikiza China kuongeza juhudi za kuidhibiti Korea Kaskazini, na ametoa pendekezo la kuwepo makubaliano bora ya kibiashara iwapo wataweza kusimamisha program ya nyuklia ya Pyongyang.

Trump wiki hii amempongeza Rais wa China Xi Jinping baada ya Beijing kurudisha meli za Korea Kaskazini zilizokuwa zimebeba makaa ya mawe kwa kuheshimu vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa.

Mwezi Februari China ilipiga marufuku uingizaji wa makaa ya mawe kutoka Korea Kaskazini, ambayo ni biashara muhimu kwa kipato cha nchi hiyo. Korea Kaskazini inaitegemea China kwa asilimia 90 katika biashara zake.

Siku ya Ijumaa, Shirika la ndege la China, pia lilifuta ratiba ya ndege zake ziendazo mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang, zikieleza kuwa hakukuwa na abiria wa kutosha.

Trump na Xi walizungumza juu ya tishio la nyuklia inayotengenezwa na Korea Kaskazini katika mkutano wao hivi karibuni katika kasri ya mapumziko ya Mar-a-Lago, mali ya Rais wa Marekani, ilioko Florida. Walizungumza tena kwa simu Alhamisi. Baada ya hapo Trump alisema anaamini kuwa Xi atafanya juhudi zote kuhakikisha mgogoro huu unamalizika katika rasi ya Korea.

Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi Ijumaa alizinasihi pande zote mbili “ kujizuia na vitendo vya uchokozi na vitisho dhidi yao, iwapo kwa maneno au vitendo, na kutoifanya hali hiyo kufikia hatua ambayo haiwezi kudhibitwa au kutatuliwa.”

Wakati China inapinga program ya nyuklia ya Korea lakini pia haikotayari kuchukua za mabavu ambazo zitasabibisha kutetereka kwa amani kwenye mipaka yake na kuiongezea nguvu Marekani katika eneo hilo.

XS
SM
MD
LG