Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 19:29

Serikali ya Ethiopia yadai hali imerudi kuwa shwari Tigray


FILE - Raia wa Ethiopia akiangalia video ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed akiongea kuhusu hali ya vita, katika internet cafe Addis Ababa, Ethiopia, Nov. 26, 2020. Waandishi wa habari wanasema amri ya kudhibiti vyombo vya habari imewia vigumu kufuatilia vita Tigray.

Hali ina ripotiwa kurejea kuwa ya kawaida tena katika mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle, nchini Ethiopia baada ya mapigano ya karibu mwezi mmoja kati ya jeshi la taifa na wapiganaji wa chama cha TPLF.

Kulingana na video iliyotolewa na televisheni ya taifa kutoka mji mkuu huo, watu wanaonekana wakiendelea na maisha yao ya kawaida huku jeshi likiripoti kugundua idadi kubwa ya silaha katika jimbo hilo.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitangaza ushindi dhidi ya wapiganaji wa chama cha ukombozi wa wananchi wa Tigray TPLF mara baada ya wanajeshi wa serikali kuu kuuteka mji mkuu wa Mekelle, lakini hadi Jumatano ilikuwa vigumu kuthibitisha habari hizo kutoka mji huo wenye wakazi wapatao 500,000.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed
Waziri Mkuu Abiy Ahmed

Video iliyotolewa na Televisheni ya Taifa, ETV, inaonyesha wakazi wa Mekelle wakiendelea na maisha yao ya kawaida na kuhudhuria ibada Kanisani.

Katika mahojiano na ETV wakazi wanasema hali ya utulivu na amani imerudi kwenye mji wao.

Naye Aleme Menkussie mwanafunzi wa chuo kikuu cha Mekelle anasema walipofika kwa mara ya kwanza katika chuo hicho mwanzoni mwa mwezi Novemba ndipo vita vilianza usiku huo huo na wakawa na hofu.

Menkussie asema : "Tuliingia uwoga na kujiuliza kwanini tumekuja huku. Halafu mawasiliano yakasitishwa na hatukuweza kuwasliana tena na familia zetu. Lakini hivi sasa amani imerudi tumefurahi, usingeliwaona watu njiani ikiwa kusingekua na amani."

Wanajeshi wa Ethiopia wakiwa katika eneo la vita Tigray
Wanajeshi wa Ethiopia wakiwa katika eneo la vita Tigray

Wanajeshi wa Ethiopia pia wanaonekana njiani na wengine kwenye ghala inayosemekana kulikuwa na silaha za kila aina iliyokuwa inasimamiwa na kundi la TPLF.

Luteni Kanali Sadik Ahmed wa Jeshi la Ulinzi wa Taifa la Ethiopia anasema hawakujua kuna idadi kubwa ya silaha namna hii iliyokuwa mikononi mwa wapiganaji wa TPLF.

Luteni Kanali Ahmed, Kamanda wa jeshi la Ethiopia anaeleza : "Makamanda wetu wanatuambia hawakuwa na habari kuhusiana na silaha hizi. Hivyo sehemu kubwa ya kazi yetu hivi sasa ni kukusanya silaha zilizoachwa nyuma na wapiganaji na kuziorodhesha. Wakazi vile vile wanatusaidia na wamekua wakituletea silaha zilizokua katika nyumba zao."

Ingali ni vigumu hadi hivi sasa kuthibitisha kwa njia huru kwamba hali imerudi kuWa shuari baada ya mapigano yaliyotishia usalama wa taifa hilo la pembe ya Afrika.

Vita hivyo vimesababisha zaidi ya watu 45,000 kukimbilia nchi jirani ya Sudan na karibu watu laki 6 wa jimbo hilo tayari walikuwa wanategemea chakula na maada wa dharura kabla ya vita kuanza Novemba 4.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG