Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Februari 25, 2024 Local time: 11:07

Serikali ya Kenya yaruhusu KTN News, NTV kurusha matangazo


Kituo cha televisheni cha NTV
Kituo cha televisheni cha NTV

Muda mfupi baada ya mwanaharakati Okiya Omtata kuonyesha nia ya kurejea mahakamani, Serikali ya Kenya kupitia Halmashauri ya Mawasiliano nchini Kenya, imerejesha matangazo ya KTN NEWS na NTV.

Licha ya Jaji wa Mahakama Kuu jijini Nairobi Chacha Mwita kutoa agizo la kusitisha mara moja marufuku hiyo ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta, serikali ilionekana kupuuza agizo hilo.

Wakati huo huo runinga ya Citizen na Inooro zinazomilikiwa na Royal Media Services zimeendelea kuzimwa.

Lakini Peter Opondo, Mkuu wa Kitengo cha Uhariri, Runinga ya Citizen, ameeleza Idhaa ya Sauti ya Amerika kuwa serikali ya Kenya haijawaeleza chochote kuhusu hatua ya kuzima runinga hizo licha ya KTN News na NTV kurejeshwa hewani.

Leo Jumatatu ilikuwa siku ya saba tangia serikali ya Kenya kusisitiza kuwa vyombo vitatu vya habari nchini Kenya vitaendelea kuzimwa.

Serikali ilisema kuwa bado inaendelea na uchunguzi ili kubaini kile inachokiita ukiukaji wa agizo lake juu ya kupeperusha matangazo ya moja kwa moja kwenye hafla ya uapisho wa kiongozi wa upinzani nchini humo Jumanne.

Lakini Peter Opondo wa televisheni ya Citizen anasisitiza kuwa Shirika la Royal Media services litasubiri kuelezwa na serikali sababu za kuendelea kuzima runinga zake.

Ali Manzu ambaye ni Mhariri wa KTN News, ameeleza kuwa japo ni afueni kurejesha masafa ya runinga ya KTN News, anasisitiza serikali inaweka mfano mbaya kwa umma kwa kukiuka agizo la mahakama.

Hali kadhalika Manzu anaeleza kuwa mtizamo ambao ulimwengu ulikuwa nao kuhusu Kenya unadidimizwa na hatua za serikali ya Kenya kuingilia utendakazi na uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Victor Bwire, Afisa wa Baraza la Vyombo vya habari nchini Kenya, ameeleza Idhaa ya Sauti ya Amerika kuwa ni sharti pawepo na uhusiano mwema kati ya Serikali ya Kenya na Vyombo vya habari.

Naye Victor Bwire wa Baraza la Habari Kenya anasema hatua hii ya Serikali ya Kenya inajiri saa chache tu baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu kufanya maandamano mjini Nairobi na kuishtumu serikali kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Kenya.

XS
SM
MD
LG