Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 27, 2022 Local time: 02:29

Serikali ya Kenya yasema : 'Tumeidhibiti hali Laikipia'


Kaunti ya Laikipia, Kenya

Waziri wa Usalama wa Ndani nchini Kenya Fred Matiang’i amesema serikali imeidhibiti hali katika jimbo la Laikipia ambako taharuki ilitanda kutokana na mapigano ya kijamii.

“Tumejitolea kupambana na suala hili mara moja na halitatokea tena,” amesema Matiag’i.

Waziri aliyasema hayo Ijumaa baada ya kuzuru eneo la Ol Moran katika kaunti ya Laikipia ambako taharuki imetanda kutokana na mapigano ya kijamii kati ya maafisa wa polisi dhidi ya majangili waliojihami kwa bunduki waliovamia maeneo mbalimbali na kuwajeruhi zaidi ya watu 12 na kuwaacha mamia kutoroka makwao.

Matamshi ya Waziri Matiang’i yanajiri muda mfupi baada ya kuibuka ripoti za majangili hao waliojihami kwa bunduki kuteketeza kwa moto nyumba saba, zikiwemo mbili zinazomilikiwa na maafisa wa polisi katika eneo la Ol Moran lililokumbwa na machafuko hayo, limeripoti gazeti la Daily Nation.

Hali ya Utulivu yarejea

Waziri huyo ameeleza kuwa serikali imechukua hatua za haraka kurejesha usalama katika jimbo hilo hasa katika maeneo bunge ya Laikipia Kaskazini na Laikipia Magharibi, na kwa ushauri na viongozi wa maeneo hayo, serikali itaanza kuwapa wakazi hatimiliki kuepusha migogoro ya kila mara ya mashamba.

“Tutaangalia mambo ya mashamba, mambo ya umiliki wa mashamba haya kuhakikisha kuwa kila mtu aliyenunua shamba hapa anasaidiwa, awe na hati ya kumiliki eneo lake na hakuna mtu anamfukuza kutoka pande hii,” ameeleza waziri Matiang’i.

Wabunge wakamatwa

Vyombo vya usalama vimewakamata Jumatano Mbunge wa Tiaty William Kamket na aliyekuwa mbunge wa Laikipia Kaskazini Mathew Lempurkel kwa madai ya kupanga mikutano ya kuchochea ghasia hizo zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu kumi na wawili na kuwaacha mamia bila makao.

Wawili hao wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa. Hata hivyo, wameachiliwa kwa dhamana.

Jeshi la Kenya ni sehemu ya vikosi vya ulinzi vilivyounganisha nguvu za maafisa wa polisi kurejesha usalama katika eneo hilo la Ol Moran, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mshirikishi wa Usalama katika bonde la Ufa, George Natembeya.

Maelezo ya wakazi wa Ol Moran

Wakazi wa Ol Moran wanaieleza VOA kuwa mchakafuko hayo yana msingi wake na kuna haja ya juhudi za kijamii kukomesha utata unaoweza kutokea baadaye na kusababisha maafa kama yale yalioshuhudiwa. Benson Kamara, mwenye umri wa miaka 42 na raia wa Ol Moran anasema kuwa amelazimika kuondoka kwake kutokana na vitisho alivyopokea.

“Wako na silaha kali. Unakuta mtu ako na bunduki aina ya M16, G3, AK47 na nyingine za rasharasha ambazo zikipigwa raia kama mimi sijawahi kushika bunduki, watoto wangu hawajawahi kushika bunduki, wanaona hakuna kitu wanaweza kufanya,”anaeleza.

Mkaazi huyo aliyepoteza mifugo yake na kulazimika kukodisha kwingineko, anaeleza kuwa bunduki haramu zilizo kwenye mikono ya wafugaji zinastahili kuondolewa.

“Mimi suluhisho ni wale ambao wako na bunduki haramu, yule aliye na bunduki haramu kinyume cha sheria za Jamhuri ya Kenya, wenye wameshika aina ya M16, wahakikishe wanazirejesha kwa serikali, ambazo wanazitumia kuwaua wananchi ambao hawana hatia. Zile bunduki ziokotwe, wakae bila hizo bunduki,” anasisitiza.

Muathirika wa mapigano

George Wainaina, mwenye umri wa miaka 32, na mkulima katika eneo la Dam Samaki, anaeleza kuwa amepoteza mali zake katika machafuko haya yaliodumu zaidi ya wiki moja.

“Kama juzi walivamia saa mbili. Jana wamevamia hapa tena. Sasa tunashindwa mahali tunakaa ni pahali aina gani. Tunakaa dunia gani hii yenye hatukai na amani tumefurushwa kwetu na pahali tunatorokea na usalama tena huko shida imetokea, hatujui tutarokea wapi,” anaeleza.

Vyanzo vya habari hii ni Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi, na gazeti la Daily Nation la Kenya

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG