Huku Sassou akiendelea kushikilia madaraka kwa nguvu zote, wanadiplomasia na wachambuzi wana mashaka iwapo yeyote kati ya wapinzani wake sita ataweza kumuondoa katika utawala wake.
Mpinzani mkuu wa rais, waziri wa zamani wa serikali Guy-Brice Parfait Kolelas, alikuwa amelazwa hospitali kutokana na COVID-19 na huenda akasafirishwa kwenda Ufaransa Jumapili, mkurugenzi wa kampeni ya Kolelas ameiambia Radio France Internationale.
Hata hivyo, inaelekea serikali haitaki kubahatisha kitu chochote. Huduma za intaneti zilizimwa kote nchini humo Jumapili, kulingana na kampuni ya iinayofuatilia huduma hiyo ya NetBlocks,
Sassou, askari wa zamani wa miavuli mwenye umri wa miaka 77, aliingia madarakani mwaka 1979. Alishindwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi huko Congo mwaka 1992 lakini akarejea madarakani mwaka 1997 baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Baadae alibadilisha katiba kuongeza muda wa kutawala.
“Ni matuamini yangu uchaguzi utakuwa wa utulivu na hakutakuwa na matukio yoyote,” amesema Michel Bedo, mstaafu mwenye umri wa miaka 80, baada ya kupiga kura kwenye shule moja katika mji mkuu wa Brazzaville. “Wananchi wa Congo hawataki ghasia yoyote itokee.”
Waangalizi wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya hawakukaribishwa kufuatilia uchaguzi, na wizara ya mambo ya ndani ilikataa kuwaruhusu waangalizi 1,100 wa Kanisa Katoliki kufuatilia nchini uchaguzi huo.
Wafuatiliaji wa uchaguzi wana matumaini, hata hivyo, kuwa upigaji kura utakuwa wa amani – kinyume na ule wa mwisho wa mwaka 2016 uliokuwa umegubikwa na ghasia. Serikali ilisaini makubaliano ya amani na kikundi cha waasi kinachompinga Sassou mwaka 2017, na kuzima vita iliyokuwepo upande wa kusini mwa Congo.
Congo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta, lakini asilimia 41 ya wakazi wake milioni 5.4 wanaishi katika kiwango cha umaskini duniani, kulingana na Benki ya Dunia.