Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, aliyekuwa afisa wa soka Patrice Edouard Ngaissona na Alfred Yakatom ambaye ni kiongozi wa uasi anayejulikana kama Rambo, wanatuhumiwa kuhusika kwenye mauaji, mateso pamoja na mashambulizi dhidi ya raia.
Mashtaka hayo ni kutokana na nafasi zao za uongozi kwenye kundi la uasi la kikristo la anti-Balaka lililoshutumiwa kuhusika kwenye mapigano makali na kundi la kiislamu la Seleka kati ya mwaka 2013 na 2014.
Mapambano hayo yalisababisha vifo vya maelfu ya watu huku maelfu wengine wakikoseshwa makazi wakati misikiti pamoja na maduka yakiporwa.
Mashtaka ya Jumanne ndiyo ya kwanza mbele ya ICC yanayoangazia ghasia zilizotokea baada ya kundi la Seleka kutwaa madaraka 2013 yaliyopekea Rais wa wakati huo Francois Bozize kutorokea uhamishoni.
-Imetayarishwa na Harrison Kamau, VOA, Washington DC