Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 14:45

Rwanda yasema kifo cha Mudacumura wa FDLR ni bishara njema


Sylvestre Mudacumura, Picha kwa hisani ya Mahakama ya ICC
Sylvestre Mudacumura, Picha kwa hisani ya Mahakama ya ICC

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Balozi Olivier Nduhungirehe amesema kuwa kifo cha kamanda wa kikundi cha waasi wa FDLR Sylvestre Mudacumura ni bishara njema ya kupatikana amani na usalama nchini DRC na katika eneo.

"Ni habari njema kwamba kutakuwa na amani na usalama nchini DRC na katika eneo lote. Na huu ni uthibitisho kuwa uongozi mpya wa Congo unatekeleza ahadi yake ya kuondoa vikundi vyote venye kuleta machafuko katika eneo la mashariki ya DRC."

Taarifa za Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimesema kamanda huyo wa kundi la waasi kutoka Rwanda Sylvestre Mudacumura, aliyekuwa anatafutwa na mahakama ya kimataifa, ICC, aliuawa usiku wa kuamkia Jumatano na Jeshi la DRC.

Wakati huohuo kifo cha kamanda wa waasi wa FDLR, Sylvestre Mudacumura kimepokelewa kwa hisiya mseto na upande wa watetezi wa haki za binadamu katika jimbo la kivu kaskazini.

Omar Kavota, mwanaharakati wa haki za binadamu katika wilaya ya Rutshuru ambayo ni ngome ya waasi hao kutoka Rwanda, anasema usalama utapatikana baada ya muasi huyo kuuawa.

“Ingawa kifo cha mwanadamu hakiwezi kufurahiwa, tunafikiri kifo cha muhalifu huyo wa kivita kitasaidia kuleta usalama katika maeneo ya kivu kaskazini.”

Lakini Placide Nzilamba, ambaye anaongoza shirika la haki za binadamu CIDHOP, anasema ilikuwa bora muasi huyo afikishwe mahakamani kujibu mashtaka dhidi yake.

“Kama shirika la kutetea haki za binadamu, sisi tulikuwa tunasubiri akifishwe mahakamani. Hivi sasa kamanda huyo wa FDLR ameuawa, kuna taarifa nyingi ambazo hazitajulikana. Tunaona ilikuwa vyema jeshi la Congo limkamate na limfikishe mbele ya mahakama.”

Mahakama ya ICC, ilitoa ilani ya kutaka Mudacumura akamatwe, mnamo mwaka 2012, kwa kudaiwa kuongoza mashambulizi dhidi ya raia, mauaji, unajisi na mateso, mashariki mwa DRC.

Kundi hilo limekuwa likitekeleza shughuli zake mashariki mwa DRC tangu mwaka 1994, tangu kutoka mauaji ya halaiki ya watu katika nchi jirani ya Rwanda.
Mudacumura alikuwa naibu wa kamanda wa kikosi cha ulinzi wa Rwanda wakati wa mauaji ya halaiki 1994, kabla ya kutorokea DRC, na waliokuwa maafisa wa ngazi ya juu katika usalama wa Rwanda.

Kundi la FDLR, limekuwa likifanya mashambulizi ya kila mara dhidi ya serikali na raia wa DRC.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG