Katika taarifa kwa vyombo vya Habari, Iwacu imesema, “tunayo masikitiko kuwatangazia Warundi na jumuiya ya kimataifa kwamba mahakama ya rufaa imetupilia mbali rufaa yetu. Wanahabari wetu watasalia gerezani.”
Wanahabari wetu hawana hatia juu ya mashtaka yaliowakabili, tutaendelea kuomba haki itendeke na tutawasilisha kesi kwenye mahakama ya juu, limeongeza gazeti la Iwacu.
Wanahabari hao walikamatwa mwezi Oktoba mwaka 2019, wakielekzea kufanya uchunguzi kuhusu Habari ya shambulizi la kundi la waasi, katika mkoa wa magharibi mwa Burundi, Bubanza.
Baadae waendesha mashtaka waliwashutumu wanahabari hao kushirikiana na kundi la wahalifu, jambo ambalo waliendelea kukana.
Januari mwaka 2020, Mahakama ya mkoa wa Bubanza iliwahukumu kifungo cha miaka miwili na nusu na kila mmoja kulipa faini ya million 1 pesa za Burundi.
Shirika la haki za binadamu Amnesty International limeeleza masikitiko yake juu ya hatua hiyo ya mahakama ya rufaa, likisema haki haikutendeka kamwe.
Amnesty International inapendekeza wanahabari hao waachiwe huru bila masharti yoyote.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Patrick Nduwimana, Washington, DC.