Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Septemba 19, 2024 Local time: 15:13

Ripoti za unyanyasaji wa wanawake zaongezeka Ulaya


Unyanyasaji wa kijinsia.
Unyanyasaji wa kijinsia.

Mkuu wa ofisi ya Bara la Ulaya ya Shirika la Afya Duniani, WHO, Hans Kluge anasema shirika lao linakerwa sana na ripoti za kuongezeka sana ghasia nyumbani dhidi ya wanawake, wanaume na watoto katika kanda hiyo ikiwa ni pamoja na Ubelgiji, Uingereza, Ufaransa, Rashia na Hispania.

Ghasia hizi zimeongezeka hususan wakati huu wa janga la corona. Kluge anasema ingawa hakuna takwimu za kutosha lakini kote barani ulaya ripoti za wanawake kunyanyaswa nyumbani zimeongezeka kwa asili mia 60.

Akizungumza na waandishi habari hii leo Hans Kluge amesema simu katika vituo vya kuomba msaada, zimeongezeka mara tano katika takriban nchi zote za Ulaya. Ameonya kamba kuendelea na hatua kali za kuwazuia watu nyumbani kutokana na janga la corona kutaweza kuwa na athari mbaya kwa wanawake walio hatarini na watoto.

Amesema ikiwa hatua hizo zitaendelea kwa miezi sita , basi wanatarajia kupata karibu kesi milioni 31 za ghasia kuhusiana ugomvi wa jinsia kote duniani, akitaja takwimu kutoka shirika la idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa.

Kluge anasema ghasia baina ya watu huongezeka wakati wa aina yoyote ya dharura, na hivyo kuwataka viongozi kuchukulia kwamba ni jukumu lao kuhakikisha idara za kuwasaidia watu zinapatikana katika miji na vijiji.

Anasema kuna baadhi ya nchi ambazo zimeshaanza kuchukua hatua kukabiliana na mzozo huo wa dharura kwa mfano Itali imetengeneza app au program kwenye simu ambapo watu wanaweza kuomba msaada bila ya kupiga simu.

Pia huko Ufaransa na Uhispania watu wanaweza kuarifu maduka ya dawa ikiwa kuna matatizo nyumbani kwa kutumia maneno maalum. Kluge anasema idadi hiyo iliyoripotiwa ni ndogo sana kwa sababu watu wanaonyanyaswa aghlabu wanaogopa kuwasilisha mashtaka yao.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG