Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 23:10

Ramaphosa asema Tutu ni 'dira yetu ya maadili na umakini wa kitaifa'


Mazishi ya kitaifa ya Askofu Mkuu hayati Desmond Tutu katika Kanisa la Mtakatifu George, Cape Town, Afrika Kusini, January 1, 2022.
Mazishi ya kitaifa ya Askofu Mkuu hayati Desmond Tutu katika Kanisa la Mtakatifu George, Cape Town, Afrika Kusini, January 1, 2022.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amempongeza marehemu Askofu Mkuu Desmond Tutu akimwita “ni dira yetu ya maadili na umakini wa kitaifa” wakati Afrika Kusini ikitoa heshima zake za mwisho katika maziko ya kitaifa Jumamosi kwa shujaa wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

“Baba yetu aliyeondoka alikuwa mpiganaji katika mapambano ya kuleta uhuru, uadilifu, kwa usawa na kwa ajili ya amani, siyo tu Afrika Kusini, nchi aliyozaliwa, lakini ulimwenguni kote,” Ramaphosa alisema, akitoa maombolezi makuu katika ibada hiyo katika Kanisa la Mtakatifu George, Cape Town, ambapo kwa miaka kadhaa Tutu alihubiri dhidi ya dhulma ya ubaguzi wa rangi.

Rais huyo alikabidhi baadae bendera ya taifa kwa mke wa marehemu Tutu, Nomalizo Leah, anayejulikana kama “Mama Leah.” Tutu, ambaye alipokea tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1984 kutokana na upinzani wake bila ya kutumia ghasia dhidi ya utawala wa wazungu wachache, alifariki Jumapili iliyopita akiwa na umri wa miaka 90.

Mkewe alikuwa amekaa katika kiti cha magurudumu mstari wa mbele kanisani, akiwa amejifunga skafu ya zambarau, rangi ya koti la uaskofu la mumewe. Ramaphosa alivaa tai iliyofanana na rangi ya skafu hiyo.

Cape Town, mji alipoishi Tutu katika sehemu kubwa ya maisha yake baadae, mvua ilikuwa inanyesha wakati siyo msimu wa masika mapema Jumamosi wakati waombolezaji walipokusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa mtu aliyekuwa maarufu kwa jina la “The Arch.”

Jua liliangaza baada ya Ibada ya kumuombea maiti huku mapadri sita waliovaa makoti meupe wenye jukumu la kubeba jeneza walisukuma jeneza nje ya kanisa kwenda katika gari ya kubeba jeneza.

Mwili wa Tutu utachomwa na majivu yake yatazikwa nyuma ya mimbari ya kanisa katika ibada binafsi.\

“Alikuwa na maumbile madogo, lakini alituzidi kwa kiwango cha maadili na imani yake,” alisema Askofu mstaafu Michael Nuttall, aliyehudumu kama naibu wa Tutu kwa miaka mingi.

Picha zenye ukubwa wa Tutu, huku mikono yake ikiwa imeshikamana, zilitundikwa nje ya kanisa, ambapo idadi ya waumini ilidhibitiwa katika mistari iliyofuata tahadhari dhidi ya COVID-19.

Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby, anayeongoza Kanisa la Anglikana duniani alisema katika ujumbe uliorekodiwa: “ Watu wamesema ‘tulipokuwa gizani, yeye ameleta mwangaza’ na kuwa … ameleta mwangaza katika nchi mbalimbali duniani zinazopambana na vitisho, migogoro, unyanyasaji na ukandamizaji.”

Familia ya Tutu walionekana kuwa na majonzi. Mtoto wake, mchungaji Nontombi Naomi Tutu, aliwashukuru wote waliowafariji kwa msaada wao wakati Ibada ya Maombi ilipoanza, sauti yake ikiwa inamajonzi.

Chanzo cha habari hii ni Shirika la Habari la Reuters

XS
SM
MD
LG