Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 09:11

Rais mstaafu wa walimu Tanzania ashikiliwa kwa tuhuma za rushwa


Rais mstaafu wa Chama cha Waalimu Tanzania, Gratian Mukoba
Rais mstaafu wa Chama cha Waalimu Tanzania, Gratian Mukoba

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania, inamshikilia Rais mstaafu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, kwa tuhuma za kutaka kuwahonga wapiga kura.

Vyanzo vya habari mjini Dodoma vimesema kuwa hatua hiyo imefuatia madai ya kuwa Mukoba alikuwa katika mchakato wa kuwashawishi wajumbe kumpigia kura mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi wa chama hicho unaofanyika Ukumbi wa Chimwaga, Dodoma mji mkuu wa Tanzania.

Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba, alisema Mukoba alikamatwa jana saa tatu asubuhi akiwa katika mchakato wa kuwashawishi wajumbe kumpigia kura mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais, ambaye jina lake hakuweza kulitaja kutokana na sababu za kiuchunguzi.

“Alionekana ukumbini akiwashawishi wajumbe wampigie kura mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais na baadae watawapa kitu kidogo,” alisema.

Misalaba alifafanua kuwa taratibu zinawaruhusu kumkamata mtu anayeonyesha viashiria vya rushwa ili kuzuia madhara kabla hayajatokea.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa elimu uchaguzi huo unafanyika wakati chama hicho kikiwa na viongozi wanaokaimu.

Nafasi ya urais anakaimu Leah Ulaya baada ya chama hicho kutoa tangazo la kusitisha ajira za Mukoba na Naibu Katibu Mkuu wake, Ezekiel Olouch.

Gazeti la Mtanzania nchini humo liliripoti karibuni kuwa Rais John Magufuli alifungua mkutano wa chama hicho na pamoja na mambo mengine, alitishia kuifuta ama kuifilisi Benki ya Walimu baada ya mwelekeo wake kutoridhisha.

Magufuli alisema benki hiyo ipo katika orodha ya benki zenye mwelekeo wa kufutwa.

XS
SM
MD
LG