Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Aprili 25, 2024 Local time: 03:59

Chama tawala Uganda cha ahidi kubadilisha katiba kwa ajili ya Museveni


Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Chama tawala nchini Uganda cha National Resistence Movement (NRM) kimeapa kuhakikisha kwamba katiba ya nchi hiyo ina badilishwa ili kumruhusu Rais Yoweri Museveni kuitawala Uganda hadi mwisho wa umri wake.

Wanasiasa wa upinzani nao wameapa kuzima kila jaribio la kuifanyia katiba marekebisho.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripori kuwa viongozi wa chama hicho tawala nchini Uganda NRM, wameapa kwamba watatumia mbinu zote kuhakikisha kwamba katiba ya nchi inabadilishwa ili kumruhusu rais Yoweri Museveni kutawala hadi kifo chake.

Japokuwa Museveni amekaa kimya, viongozi wa chama cha NRM, wanasema kwamba wanasiasa wa upinzani wanamaliza muda wao kupinga nia ya chama tawala kuondoa ibara ya 102 be inayomzuia mtu yoyote aliyetimiza umri wa miaka 75 kuwania madaraka ya urais.

Viongozi hao wanaongozwa na mshauri wa rais, David Mafabi ambaye amesema kuwa: “Hakuna wasiwasi kuhusu hilo. Tunataka katiba ibadilishwe na tunaieleza dunia ijue. wanaopinga wachunguze.

Kulingana na viongozi wa chama cha NRM, umri hauwezi kuwa kizuizi kwa kiongozi aliye na uwezo wa kuingoza nchi, na kwamba hakuna mtu yeyote nchini Uganda anayeweza kuwa rais isipokuwa Yoweri Kaguta Museveni.

Rais Yoweri Museveni ambaye ameripotiwa mara kadhaa kutojua tarehe kamili aliyozaliwa, anadai kwamba alizaliwa mwezi agosti mwaka 1945 bila kujua tarehe kamili, na ana umri wa miaka 72. Ifikapo mwaka 2021 wakati wa uchaguzi mkuu, atakuwa na umri wa miaka 76, mwaka mmoja zaidi ya inavyohitajika kikatiba.

NRM imesema kuwa: “Tunaghadhibishwa na kampeini inayoendelezwa na baadhi ya wanachama wa upinzani kuhusu maswala nyeti ya taifa kwa kutumia mbinu mbovu zikiwemo propaganda na vitisho.”

Wanasiasa wa upinzani wakiongozwa na Dkt Kiiza Besigye wa FDC na Nobert Mao, kwa upande wao, wameendeleza kampeni ya kutaka raia kususia jaribio la serikali kuifanyia marekebisho katiba wakitishia kutumia mbinu zote kuzima hatua hiyo.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa Bunge ndilo lililo na uamuzi endapo katiba itabadilishwa au la. Idadi kubwa ya wabunge ni wanachama wa NRM, chama chake Museveni.

Katiba ya Uganda ilifanyiwa mabadiliko mnamo mwaka 2005 na kuondoa kizuizi cha mihula miwili, iliyomwezesha Museveni kuwania urais kwa mara nyingine. Museveni ameitawala Uganda tangu mwaka 1986.

Imetayarishwa na mwandishi wetu wa Kampala, Kennes Bwire

XS
SM
MD
LG