Makubaliano hayo, ambayo yanaweza kusainiwa mapema wiki hii, yanaweza kumuondoa Netanyahu katika jukwaa la siasa la Israeli kwa miaka mingi, na kufungua njia kwa ushindani wa uongozi katika chama chake cha Likud na kutikisa ramani ya kisiasa ya Israeli.
Makubaliano yoyote yatakayofikiwa yatamtoa Netanyahu katika kesi ya kufedhehesha ambayo imelikumba taifa na hatari ya kubadilisha urithi wake wa kisiasa.
Msemaji wa Netanyahu alikataa kutoa maoni.
Netanyahu anashtakiwa kwa wizi, uvunjifu wa sheria ya uaminifu na kupokea rushwa katika kesi tatu tofauti. Waziri Mkuu wa zamani, hivi sasa kiongozi wa upinzani, anakataa amefanya makosa yoyote.
Mtu anayehusika na mazungumzo hayo amesema ombi hilo la makubaliano litamuondolea mashtaka ya ufisadi na wizi na kufuta kesi moja kabisa.
Mtu huyo ameomba jina lake lisitajwe kwa sababu hajaidhinishwa kujadili maelezo ya mazungumzo hayo. Amesema ombi la makubaliano huenda likatangazwa siku zijazo.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AP