Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 06, 2022 Local time: 20:15

Mwai Kibaki, Rais wa tatu wa Kenya, afariki


Aliyekuwa Rais wa tatu wa Kenya, Mwai Kibaki.

Rais wa tatu wa Kenya Mwai Kibaki aliaga dunia Ijumaa tarehe 22 Aprili, 2022, akiwa na umri wa miaka 90. Kibaki alikuwa rais wa taifa hilo la Afrika Mashariki kutoka mwaka wa 2002 hadi 2013.

Rais wa sasa wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alithibitisha kifo cha Kibaki Ijumaa katika hotuba yake kwa taifa iliyorushwa moja kwa moja kupitia televisheni na vyombo vingine vya habari.

Kibaki alihudumu kama makamu wa Rais wa Kenya chini ya Rais Daniel Arap Moi na baadaye kama waziri wa Afya hadi mwaka wa 1991 alipojibwaga kwenye siasa za mrengo wa upinzani, chini ya vuguvugu jipya la kutaka mabadiliko ya kisiasa.

"Kama mtu mashuhuri katika historia ya Kenya baada ya uhuru, Mwai Kibaki alipata heshima na mapenzi ya kudumu ya watu wa taifa hili na mataifa mengine ulimwenguni," alisema Rais Kenyatta katika hotuba yake.

“Rais Kibaki atakumbukwa milele kama muungwana katika siasa za Kenya. Alikuwa mdadisi mahiri, ambaye ujuzi wake wa ufasaha na haiba ulikuwa wa manufaa makubwa mara kwa mara," aliongeza Kenyatta.

Kibaki anakumbukwa kwa sababu ya machafuko yaliyotokea kufuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 ambapo baada yake kutangazwa mshindi, mpinzani wake wakati huo , Raila Odinga, alipinga matokeo.

Takriban watu 1,200 walipoteza maisha yao katika mapigano yaliyofuatia, huku maelfu wengine wakifurushwa makwao.

Mnamo mwaka wa 1991, Rais Kibaki aliondoka serikalini na kuongoza vuguvugu la kuiwajibisha chama tawala, baada ya kuunda chama cha upinzani cha Democratic Party, DP.

"Michango yake katika kurejesha demokrasia ya vyama vingi, kama kiongozi rasmi wa upinzani, pamoja na rekodi yake na sifa za kuvutia zilimfanya Mwai Kibaki kuchaguliwa kama mgombeaji mwafaka wa upinzani dhidi yangu mwenyewe katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2002," alisema Rais Kenyatta.

Kenyatta hakueleza sababu ya kifo lakini Kibaki lakini vyombo vya habari vya Kenya viliripoti kwamba amekuwa akiugua kwa muda.

Wanasiasa walipumzika kufanya kampeni za uchaguzi mkuu uliopangwa Agosti 9, ili kumuomboleza Kibaki.

Shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba Kibaki alishindwa kukabiliana na ufisadi uliokithiri, ambao unasalia kuwa donda sugu mpaka waleo.

Kibaki pia alikuwa amejaribu kuleta amani katika maeneo yenye mihemko ya kikanda, alisema Moses Wetengula, ambaye alihudumu katika baraza la mawaziri.

"Kama waziri wake wa mambo ya nje, niliongoza operesheni nyingi kuleta utulivu Somalia na maeneo mengine yenye y ukosefu wa utulivu ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo," Wetangula alisema.

Walinda amani wa Kenya bado wanahudumu kusini mwa Somalia.

WASIFU

Kibaki alizaliwa mwaka wa 1931 katika kijiji cha Thunguri ,tarafa ya Othaya ya Kenya iliyokuwa Wilaya ya Nyeri, ambayo sasa ni Kaunti ya Nyeri.

Hapo awali alihudumu kama Makamu wa nne wa Rais wa Kenya kwa miaka kumi kutoka 1978 hadi 1988 chini ya Rais Daniel arap Moi.

Pia alishikilia nyadhifa za mawaziri katika serikali za Mzee Kenyatta na Moi, ikijumuisha wakati mmoja kama waziri wa Fedha (1969-1981), na Waziri wa Mambo ya Ndani (1982-1988) na Waziri wa Afya (1988-1991) chini ya Moi. 2]

Kibaki aliwahi kuwa Mbunge wa upinzani kuanzia 1992 hadi 2002. Aligombea urais bila mafanikio mwaka 1992 na 1997.

Aliwahi kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuanzia 1998 hadi 2002. Katika uchaguzi wa urais wa 2002, alichaguliwa kama rais wa tatu wa nchi hiyo.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG