Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 12:06

Museveni awaonya wanasiasa, waandishi wa habari Uganda


Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amewaonya wanasiasa na waandishi wa habari kuwa watakabiliwa na nguvu zote za dola endapo watajihusisha na vitendo vya uchochezi dhidi ya serikali.

Museveni amedai ni uchochezi kwa makundi hayo kueneza chuki kuhusu azimio la kubadilisha katiba.

Pia amesema kwamba wakati mwafaka utakapofikiwa, atafanya maamuzi yake kuhusu katiba ambayo wengi hawatapendelea.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti Alhamisi kuwa baada ya kimya cha muda mrefu, hatimaye rais wa Uganda Yoweri Museveni amezungumzia kuhusu harakati zilizopo kubadilisha katiba hatua ambayo wachambuzi wa kisiasa wanasema inalenga kumsaidia kusalia madarakani.

Akionekana mwenye hasira, Museveni amesema kwamba amekuwa akisikia watu wakizungumzia kuhusu katiba kubadilishwa, lakini hana muda kuulizia kwa kina wanazungumzia nini, akisisitiza kwamba atakapofanya maamuzi yake, wanaojadili swala hilo hawatafurahia.

Museveni alifanyia marekebisho katiba ya Uganda mwaka 2005 na kuondoa kizuizi cha mihula miwili kwa kiongozi wa taifa.

Tangia kipindi hicho, amekuwa akiwania urais na kusalia madarakani japo wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakidai kwamba hufanya udanganyifu mkubwa katika hesabu za kura.

Lakini hivi sasa, umri unamzuia kuwania tena ifikapo mwaka 2021, kwani atakuwa ametimiza miaka 76 wakati katiba inaweka kizuizi kuwa miaka 75.

Wakati Museveni akieleza azimio hilo la kuifanyia marekebisho katiba, waziri wake wa uekezaji Anite Everline amedai kupokea vitisho vya kuuawa kwa kuwa yuko mstari wa mbele katika kafanikisha azimio hilo.

“Wamenitishia maisha na hata kutishia maisha yangu kwamba wataniua. Lakini nimewaeleza kwamba nitakufa leo, nao watakufa kesho,” amesema waziri huyo.

Wanasiasa wa upinzani nao wameapa kuhakikisha kwamba ibara ya 102b haifanyiwi mabadiliko kuondoa kizuizi cha umri kwa wagombea urais.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Uganda.

XS
SM
MD
LG