Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 17:48

Msumbiji bado inakabiliwa na ukosefu wa msaada wa kibinadamu


Watu wakisubiri kupokea resheni ya chakula nje ya kambi ya watu waliolazimika kuhama makazi yao baada ya kunusurika wakati kimbunga Idai kilipopiga Msumbiji, April 4, 2019.
Watu wakisubiri kupokea resheni ya chakula nje ya kambi ya watu waliolazimika kuhama makazi yao baada ya kunusurika wakati kimbunga Idai kilipopiga Msumbiji, April 4, 2019.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaripoti kuwa Msumbiji bado inakabiliana na athari za uharibifu ulioletwa na kimbunga Idai, ambao ulisababisha janga la kibinadamu ambalo linaendelea hadi hii leo.

Kimbunga Idai, moja ya vimbunga vilivyokuwa na athari mbaya sana Afrika, kilipiga katikati ya Msumbiji mwaka moja uliopita, na kuua zaidi ya watu 1,300 na kuwaacha mamia kwa maelfu ya watu bila makazi. Kilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na kuangamiza maisha ya mamilioni ya watu.

Walionusurika katika janga hilo wanaendelea kuwa na maisha magumu kuweza kumudu maisha yao tena.

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa watu milioni 2.5, nusu ya hao watoto, wanahitaji msaada wa kibinadamu ili kuendelea kuishi.

Shirika la Chakula Duniani (WFP) inaripoti jamii katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula kwa sababu ya ukame uliodumu kwa muda mrefu. Pia, shirika hilo linasema hali inaendelea kuwa mbaya kwa idadi ilioongezeka ya watu waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya uvunjifu wa amani na vikundi venye misimamo mikali upande wa kaskazini.

Msemaji wa WFP Elizabeth Byrs ameiambia VOA shirika lake halina fedha zitakazo wawezesha kufanya ujenzi wa maeneo muhimu yaliyoharibiwa na kimbunga. Anasema mwezi Februari WFP ililazimika kupunguza resheni kwa asilimia hamsini kwa zaidi ya nusu milioni ya watu wanaofanya kazi katika miradi ya kufufua maeneo yaliyoharibiwa na kimbunga.

BYRS anasema : “Mwezi huu wa Machi, tulilazimika kusitisha kabisa kutoa resheni za misaada. Na kwa sababu hii tunawasiwasi na upatikanaji wa fedha kukabiliana na hali hii, kwa sababu hatuwezi tena kuwasaidia wakulima wadogo wadogo ambao wamepoteza mazao yao na hawawezi kulima tena. Hivyo basi wanahitaji kazi hizi za miradi ya kufufua miundombinu na chakula kwa ajili ya kusaidia katika ujenzi ili waweze kuendelea na maisha yao.”

WFP inaomba dola za Marekani milioni 91 kutekeleza mpango wa miradi ya kutengeneza miundombinu iliyoharibika kwa manusura wa Idai mwaka 2020. Fedha pia inahitajika kwa dharura kukabiliana na utapiamlo unaoongezeka.

UNICEF inaripoti kuwa hali ya utapiamlo ni mbaya sana na tayari inawaathiri asilimia 43 ya watoto ambao ni chini ya miaka mitano, moja ya kiwango cha juu kabisa duniani. Imeongeza kusema zaidi ya watoto 3,000 chini ya miaka mitano wamekutikana na hali mbaya ya utapiamlo inayohatarisha maisha yao baada ya mavuno kuangamizwa na mafuriko.

WFP inasema watoto hawapati chakula cha kutosha na wanakosa virutubisho kuwafanya waweze kuwa na afya. Inasema kujitokeza kwa tatizo hili kubwa ni mlipuko ambao ni nadra kutokea wa ugonjwa wa pellagra, unaosababishwa na ukosefu wa vitamin B3.

Shirika hilo linasema watu 4,000, wengi wao watoto, wameathiriwa na maradhi haya ambayo husababisha kuharisha, vipele na ukosefu wa kumbukumbu, ni hatarishi kama haujatibiwa.

XS
SM
MD
LG