Nchi ya Malawi imekumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu, miezi miwili tu baada ya msimu wa mvua kuanza. Mamlaka za Afya nchini humo zinasema ugonjwa huo umeathiri wakaazi wengi katika wilaya tatu zinazozingira ziwa Malawi.
Milipuko ya kwanza ya kipindupindu iliripotiwa katikati ya mwezi katika Machinga na Zomba mashariki mwa wilaya za Machinga na Zomba ambako mtu mmoja alifariki na wengine 26 kulazwa mahospitalini.
Maafisa wa Wizara ya Afya nchini Malawi waliiambia Sauti Ya Amerika Jumatano kwamba ugonjwa huo, ambao husambazwa kupitia maji, unaenea kwa kasi, huku kukiwa na visa 95 vilivyoripotiwa.
Wanasema mlipuko wa ugonjwa huo umechangiwa pakubwa na hali duni ya usafi wa mazingira katika eneo la ziwa Chilwa.
Andrian Chimbuke ni msemaji wa wizara ya afya.
Anasema: “Katika ziwa Chilwa, watu wana mazoea ya kujenga manyumba karibu sana na maji…halafu kuna wale wanaokuja kuvua samaki na mambo mengine..kwa hivyo hali ya usafi inaathiriwa mno.”
Wataalam wa maswala ya afya wanasema kipindupindu huenezwa kupitia kula chakula ambazo kina viini vinavyotoka kwa kinyezi na uchafu mwingine. Dalili zake ni kuhara, kutapika, na kupoteza maji mwilini.
Kuna uwezekano mkubwa kwa wale wasiopata matibabu ya haraka kufa kwa muda wa masaa ishirini na manne.
Nchini Malawi kuna wasiwasi kwamba maradhi haya huenda yakaenea hadi wilaya zingine iwapo hayatadhibitiwa.