Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 08, 2023 Local time: 03:09

Mjadala juu ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kumalizika Ijumaa


Wajumbe wa Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wa Umoja wa Mataifa (COP26), Glasgow, Scotland, Uingereza, Nov. 12, 2021.
Wajumbe wa Mkutano wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa wa Umoja wa Mataifa (COP26), Glasgow, Scotland, Uingereza, Nov. 12, 2021.

Mazungumzo juu ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa yanatarajiwa kumalizika Ijumaa baada ya wiki mbili za majadiliano ya dhati bila ya kufanikiwa kutanzua baadhi ya mivutano muhimu. 

Wajumbe hawakuweza pia kupendekeza mipango inayohitajika kupunguza gesi chafu ili kuzuia kuongezeka kwa joto duniani kwa zaidi ya nyuzi 1.5 Celsius.

Ingawa viongozi wa dunia wamependekeza mipango kadhaa lakini wataalamu, wanaharakati na hata Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wanasema mipango hiyo haitoshi kupunguza joto.

Katibu Mkuu Antonio Guterres
Katibu Mkuu Antonio Guterres

Baada ya wiki mbili za majadiliano mfululizo wajumbe kutoka karibu mataifa 200 wameweza kutoa rasimu ya taarifa ya mwisho juu ya maendeleo yao hii leo.

Taarifa hiyo ya COP26 inatoa wito kwa serikali za dunia kuharakisha juhudi za kufunga vinu vya umeme vinavyotumia mkaa na kuzuia kutoa ruzuku kwa ajili ya mafuta ghafi yanayotoka chini ya ardhi.

Licha ya ahadi kubwa za kulinda misitu na kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, lakini hakuna maendeleo yaliyoweza kupatikana katika majadiliano ya kiwango cha waatalamu na kile cha mawaziri kwa hivi sasa.

Waatalamu na wanaharakati hasa vijana wanaelezea wasiwasi wao kuhusu kutopatikana maendeleo na athari zinazoyakabili mataifa yanayoendelea ambayo hayachangii sana katika uchafuzi wa hewa.

Mwanahaklati wa Uganda Vanessa Nakate katika hotuba yake ya kusisimua jana amesema kwa miaka 25 viongozi wamekuwa wakitoa ahadi lakini hakuna kilichobadilika.

Wataalamu wanasema ahadi mpya zilizotolewa na viongozi kwenye mkutano huo ikiwa zitatekelezwa kwa ukamilifu zitaweza kupunguza kuongezeka hali ya joto hadi chini ya nyuzi joto mbili, kiwango kilichowekwa kwenye mkataba wa Paris wa 2015

Lakini wanaharakati na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres wakizungumza jana wanasema ahadi hizo hazitoshi.

“Tungali katika njia ya hatari ya kuongezeka sana hali ya joto kuzidi nyuzi joto mbili celsius, kwa hivyo ahadi za kufikia sifuri zinahitaji upunguzaji endelevu za uchafuzi wa hewa muongo huu,” Guterres amesema.

Mjumbe maalum wa hali ya hewa wa Marekani John Kerry aliwatia moyo wajumbe alipotangaza jumatano kwamba Marekani na China zitashirikiana katika kukabiliana na atahri za mabadiliko ya hali ya hewa na makubaliano yao ni tangazo la wazi kuhusu juhudi za lazima za kushirikiana.

Kerry amesema “tunawajibika kukabiliana na matatizo haya kwa haraka zaidi, inatulazimu kupunguza haraka uzalishaji wa gesi ya Methane, tunabidi kuendelea kuongeza matarajio yetu hasa kuchukua hatua kuhakikisha ongezeko la joto halizidi nyuzi joto 1.5 za celsius.”

Mkutano wa Glascow unamalizika bila ya kuwaridhisha wanaharakati wanaosema mambo ni yale yale na waatalamu wakionya kwamba ahadi ya kutoa dola bilioni 100 kila mwaka haitotosha tena na gharama zitapanda ikiwa wataruhusu joto kuendelea kuongezeka duniani.

Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali vya habari ikiwemo AP na AFP

XS
SM
MD
LG