Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Julai 27, 2024 Local time: 04:18

Wanafunzi Burundi waishinikiza serikali kuwaachia huru wenzao


Pierre Nkurunzinza
Pierre Nkurunzinza

Wanafunzi wa chuo kikuu cha serikali nchini Burundi Alhamisi wameanza mgomo baridi wa kususia masomo wakishinikiza wenzao sita waliokamatwa na polisi waachiliwe huru bila masharti.

Wanafunzi hao waliokamatwa baadhi yao ni wajumbe wa bodi ya wawakilishi wa wanafunzi.Jana usiku wanne kati yao waliachiliwa huru.

Msemaji wa polisi Pierre Nkurikiye amesema wanafunzi hao wanazuiliwa katika gereza la idara ya upelelezi kwa tuhuma za kutaka kuanzisha vurugu kwenye chuo kikuu cha serikali. Miongoni mwao ni naibu wa kiongozi wa wawakilishi wa wanafunzi.

Hata hivyo Waziri wa Elimu Dkt Janviere Ndirahisha amesema kuwa kamwe serikali haiwezi kuachana na mageuzi hayo.

"Wapende au wasipende kuanzia mwaka wa masomo ujao hakuna msaada wa pesa utakatolewa kwa wanafunzi, bali watapewa mkopo ambao watalazimika kuulipa," amesema waziri huyo.

Kwa mjibu wa polisi wanafunzi wanadaiwa kuanzisha vurugu ndani ya chuo kikuu. Hii ni baada ya kusaini, wakiwa pamoja na wengine 170, waraka walioutuma kwa rais wa Burundi wakitishia kugoma, kwa ajili ya kupinga mageuzi yanayotaka kuletwa kwenye chuo hicho.

Kwa mujibu wa waraka huo, mgomo wa kupinga mageuzi hayo umepangwa kuanza tarehe nne mwezi Aprili.

Mageuzi hayo ni kusitishwa kwa mpango wa serikali wa kuwapa msaada wa pesa wanafunzi na badala yake wapewe mikopo kuanzia mwaka mpya ujao wa masomo.

Kwenye matawi matatu ya chuo kikuu cha serikali hapa jijini Bujumbura, idadi ndogo ya wanafunzi ndio waliojitokeza alhamisi kuhudhuria masomo.

Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Idhaa ya Kiswahili VOA wamedai kuwa wamekuja kufanya mitihani huku wengine wakidai kuwa wamekuja kupokea posho yao ya kila mwezi.

Ingawa hakuna aliyekiri kuwa ni mgomo rasmi, hali hii imefuatia wito uliotolewa jana na wawakilishi wa wanafunzi.

Chuo kikuu cha serikali kina zaidi ya wanafunzi elfu kumi na moja na mgomo unatarajiwa wakati ambapo wadadisi wanasema uhuru wa kujieleza umebanwa na si wakati mwafaka wa kuwasilisha malalamiko kupitia njia za migomo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Haidallah Hakizimana, Burundi

XS
SM
MD
LG