Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 04:05

Mgogoro wa uhaba wa mafuta Afrika Mashariki wapelekea mfumuko wa bei


Solai Kenya
Solai Kenya

Imekuwa ni wiki ya matatizo huko Afrika Mashariki, ambako kumekuwepo na uhaba wa mafuta na mfumuko wa bei za bidhaa kwa wanunuzi, huku eneo hilo likiendelea kutikiswa na tatizo la COVID-19 katika kufufua uchumi wa taifa.

Maeneo mengi hivi karibuni yamekumbwa na uhaba wa petroli na yanapopatikana, bei zimepanda kwa viwango vikubwa sana.

Gharama ya maisha imepanda. Mfumuko wa bei uko asilimia 6.29 nchini Kenya, 3.2% nchini Uganda , 4.2% nchini Rwanda, 3.8% nchini Tanzania, 13.3% Burundi ,asilimia 25 Sudan Kusini na asilimia 5 Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mfumuko wa Bei

Nchini Uganda, ambako usambazaji mafuta umevurugika tangu Januari, kuna maeneo ambako lita ya petroli inagharimu dola 3. Kenya ilikumbwa na uhaba wiki iliyopita, ikidumaza huduma za usafiri wa umma. Wafanyabiashara wanadai kuwa uhaba huo ulipelekea kuongezeka kwa bei za bidhaa zinazouzika haraka.

Nchini Kenya, uhaba wa mafuta unalaumiwa kwa serikali kushindwa kuwalipa waagizaji wa mafuta ruzuku yao.

Hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusaini bajeti ya nyongeza kwa malipo ya shilingi bilioni 34 za Kenya ($298 milioni) kwa Mfuko wa Kodi ya Maendeleo ya Petroli (PDLF), uhaba huo umeendelea huku kukiwepo mivutano juu ya kiwango ambacho serikali inatakiwa kuyalipa makampuni ya mafuta.

Maafisa walisema ni shilingi bilioni 13 za Kenya ($112 milioni), lakini kampuni hizo zinasema wanadai zaidi ya shilingi bilioni 20 za Kenya ($173 milioni)

Wizara ya Mafuta

Kiasi cha shilingi bilioni 8.2 za Kenya ($71.1 milioni) zilitolewa kwa makampuni hayo Jumatatu kulipa sehemu ya deni hilo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mafuta Andrew Kamau alisema kuwa serikali inatathmini kiwango gani kinadaiwa na mchakato huo unaweza kuchukua zaidi ya mwezi mmoja.

Baadhi ya waagizaji bidhaa hiyo wameendelea kuhodhi mafuta wakisubiri tathmini ya bei kila mwezi inayofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli Aprili 14, wakitumaini bei ya mafuta kuwa juu zaidi.

Katika bajeti ya nyongeza ambayo ilisainiwa na Rais Kenyatta Aprili 4, aliidhinisha shilingi bilioni 34.4 za Kenya ($298.3 milioni) zilizotengwa kwa ajili ya PDLF ili kuimarisha bei na kumaliza mgogoro huo.

Afrika Mashariki

Kulikuwa na ongezeko la bei ya mafuta katika vituo vya kuuzia katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, huku serikali mbalimbali zikilaumu hali hiyo imetokana na uvamizi wa Russia nchini Ukraine mwishoni mwa Februari, iliyopelekea kuvuruga mtiririko wa usambazaji mafuta duniani na kupanda kwa gharama kote duniani

Nchini Uganda, ambapo bei ya petroli imeongezeka kufikia dola 1.4 kwa lita, raia wanataka serikali ifikirie kupunguza kodi katika bidhaa zinazotokana na petroli na kudhibiti bei za rejareja.

Waganda wanaoishi karibu na mpaka wa Tanzania wamekuwa wakivuka mpaka kununua petroli iliyo bei ya chini , hususan upande wa kusini mwa mpaka wa Mutukula.

Wiki iliyopita, Tanzania iliongeza bei ya mafuta katika vituo vya kuuzia mafuta kwa zaidi ya asilimia 11 kwa bidhaa ya petroli na dizeli, na asilimia 21 kwa mafuta ya taa.

Kulingana na bei zilizotangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuanzia Aprili 6, bei ya petroli na dizeli iliongezeka kwa shilingi 321 za Tanzania ($0.14) hadi shilingi 2861 za Tanzania ($1.23) na shilingi 289 za Tanzania ($0.12) hadi shilingi 2,692 za Tanzania ($1.16) kwa lita.

Chanzo cha habari hii ni gazeti la The East African, Kenya

XS
SM
MD
LG