Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 22, 2024 Local time: 10:45

Polisi waanzisha msako mkali wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji


Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba

Jeshi la Polisi limeanza rasmi kuwasaka watuhumiwa 12 wa mauaji ya Polisi na raia katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, Mkoa wa Pwani nchini Tanzania.

Jeshi hilo aidha limetangaza kumzawadia mtu yoyote Sh milioni 5 atakayefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni pamoja na Abdulshakur Makeo aliyetajwa kuwa ni mwanzilishi wa harakati za mauaji Ikwiriri, wilayani Rufiji.

Wengine ni Faraj Nangalava, Anaf Kapera pia anafahamika zaidi kama Kapelo, Said Ngunde, Omar Matimbwa, Shaaban Kinyangulia, Haji Ulatule, Ally Ulatule, Hassan Uponda, Rashid Mtulula, Shehe Hassan Mzuzuri na Hassan Njame.

“Jeshi la Polisi mkoani Pwani limefanya jitihada kubwa kwa kushirikiana na wasiri wetu kuwabaini watuhumiwa wa vitendo vya mauaji vinavyoendelea katika mkoa wetu hususan wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga.

”Watuhumiwa hawa hupendelea kutembelea maeneo ya kisiwa cha Simbaulanga, kisiwa cha Saninga, Kijiji cha Nchinga, Kijiji cha Mfesini katika Kata ya Nyamisati na maeneo mbalimbali ya wilaya za Kibiti, Rufiji na Mkuranga,” amesema kamanda Lyanga.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba akizungumza bungeni hivi karibuni alisema Serikali inalichukulia matukio hayo kwa uzito mkubwa ili kuhakikisha wanarejesha hali ya usalama katika maeneo hayo na nchi nzima.

Alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu wananchi na kusema kuwa matukio hayo yameipa Serikali chachu zaidi ya kupambana na uhalifu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa katika mazingira salama.

XS
SM
MD
LG