Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 09:16

Mashishanga asema wananchi Mkuranga, Rufiji na Kibiti wanahofu kubwa


Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba
Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba

Wakati wananchi wa Wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti wakiwa wamegubikwa na hofu na wasiwasi mkubwa, kufuatia mauaji yaliyofanyika katika maeneo hayo hivi karibuni, serikali ya Tanzania imetakiwa kufanya uchunguzi wa kina.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Stephen Mashishanga amesema vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha mauaji hayo yanakomeshwa mara moja.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi nchini Tanzania hivi karibuni mstaafu huyo ameongeza kauli yake juu ya kauli za wananchi wa mkoa wa pwani ambapo amesema wananchi wanaendelea kuishi kwa hofu ya kutofahamu nani atafuata katika orodha ya wanaosakwa kuuawa.

“Ni aibu kwa kinachoendelea. Serikali iangalie imekosea wapi au wananchi wake wamefanya nini hadi hali hiyo ikatokea na ikomeshe matukio hayo,” alisema Mashishanga, ambaye kwa nafasi ya ukuu wa mkoa alikuwa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama.

Kwa uzoefu wake, alisema huenda dhuluma ikawa chanzo hivyo uchunguzi ufanywe haraka na kurekebisha kasoro zitakazobainika ili wananchi wa mkoani humo waishi kama ilivyo maeneo mengine.

“Wakati mwingine viongozi wanajisahau katika maamuzi yao. Bila kujua wanaweza wakawa wanapandikiza chuki na kusababisha kisasi ambacho kinaweza kuhusisha vifo vya namna hii,” Mashishanga alieleza shaka yake.

Maeneo yenye kuweza kusababisha mauaji hayo mkuu huyo wa zamani wa mkoa amesema ni masuala ya uhusiano hasa wa ndoa, mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya vyama kwa ngazi za wilaya au uporaji mali kwa kutumia mamlaka.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari mkoa wa pwani, kuna orodha ya watu ambao majangili hao wanawatishia wakiwemo wanasiasa katika ngazi za wilaya na hata taifa.

"Mimi ninaishi hapa Kibiti lakini hali sio shuari kwani kuna wasiwasi mkubwa hasa kwa upande wa viongozi kupoteza maisha yao," mkazi ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia VOA Jumamosi.

"Hivi tunavyo ongea watu wenye ndugu zao nje ya mkoa wa pwani wameanza kuondoka kwa hofu ya kulazimishwa kutoa taarifa ambazo hawazijui kwa vyombo vya dola au kuwa mhanga iwapo majangili hao watajua unashirikiana na polisi," amesema.

Juhudi za kuwapata viongozi wa wilaya zote tatu na wabunge ziligonga ukuta siku ya ijumaa baada ya kuwa simu zao zilikuwa hazipokelewi.

Lakini wakati huo huo jeshi la polisi limeendelea kuimarisha ulinzi katika mkoa wa pwani na vikosi zaidi vimepelekwa katika maeneo yenye utata ya wilaya hizo tatu.

Wananchi wamesema kuwa ulinzi umeimarishwa japokuwa bado hofu imetanda kwa wananchi.

Mkazi mwengine wa Rufiji ambaye alitaka jina lake lihifadhiwe amesema kuwa watu wanaogopa kwenda katika shughuli hata za msiba.

Wakati watu wasiojulikana wakiendelea kuua viongozi wa vijiji licha ya Jeshi la Polisi kuweka kambi, wananchi waliozungumza na VOA wamesema Serikali ijitathmini, kwani matukio hayo ya mkoani Pwani yanaitia doa.

Watu 31 wameshauawa katika kipindi cha kuanzia Mei mwaka jana na mauaji ya viongozi wa vijiji yamekuwa yakishabihiana, na pia matukio kadhaa ya askari wa Jeshi la Polisi kuuawa katika mashambulizi.

Mpaka sasa viongozi 15 wa serikali za vijiji na vitongoji vya wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti, polisi kumi, watumishi wawili wa Idara ya Maliasili, mwanachama mmoja wa CCM na watu watatu waliokuwa wamevaa nguo za kike wameshauawa katika kipindi hicho.

Hadi sasa, Jeshi la Polisi halijaeleza kama wanaofanya mauaji hayo katika vijiji hivyo, ambavyo baadhi vinapakana na hifadhi za taifa, ni majambazi, magaidi au majangili.

“Hatupendi kuona haya yanayotokea yakitendekea na kuendelea kusikika kila siku kana kwamba hatuna vyombo imara vya ulinzi na usalama,” alisema Mashishanga alipozungumza na gazeti la Mwananchi huko Arusha.

Jeshi la Polisi limeweka kambi katika Kijiji cha Jaribu katika jitihada za kukabiliana na mauaji hayo na Wizara ya Mambo ya Ndani imetangaza katika bajeti yake ya mwaka 2017/18 kuwa itaunda mkoa maalumu wa kipolisi utakaojumuisha wilaya hizo tatu.

Hata hivyo wananchi na wanasiasa wameendelea kuwa na wasiwasi kutokana na vitendo vya mauaji kuendelea baada ya makada wawili wa CCM kuuliwa na watu wawili wengine kujeruhiwa tangu Waziri Mwigulu Nchemba atangaze uamuzi huo.

Katika tukio la wiki hii, watu wasiojulikana walimuua kwa risasi mwenyekiti wa CCM wa Tawi la NjiaNne, Iddy Kirungi aliyekuwa akijaribu kukimbia baada ya kuwaona wauaji waliokuwa wamemjeruhi mtoto wake.

Mtoto huyo alikuwa akielekea bafuni na inaonekana wauaji walidhani kuwa ni mwenyekiti huyo na kumrushia risasi. Siku tano kabla ya tukio hilo, watu hao walimuua kwa risasi aliyekuwa katibu wa CCM wa Kata ya Bungu, Alife Mtulia wakati akielekea bafuni kuoga.

XS
SM
MD
LG