Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 17, 2024 Local time: 06:09

Marekani iko tayari kufanya mjadala na pande zinazozozana Sudan


Moshi ukifuka katika eneo la kusini la jiji la Khartoum tarehe 29 Mei 2023, Picha na AFP.
Moshi ukifuka katika eneo la kusini la jiji la Khartoum tarehe 29 Mei 2023, Picha na AFP.

Marekani ilisema siku ya Alhamisi iko tayari kufanikisha majadiliano kati ya pande zinazozozana za Sudan iwapo pande hizo zitaonyesha nia ya dhati kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotekelezwa, yaliyokuwa yakisimamiwa na Marekani pamoja na Saudia Arabia.

"Mara tu vikosi vitakapoweka wazi kwa vitendo vyao kwamba vina nia thabiti ya kutekeleza sitisho la mapigano, Marekani na Ufalme wa Saudi Arabia wako tayari kuanza tena kufanikisha majadiliajo yaliyosimama ili kupata suluhisho kwa mzozo huu," alisema Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya jeshi la Sudan kuvunja mazungumzo na kuvishutumu vikosi vya pinzani kwa kukiuka makubaliano hayo mara kwa mara.

Pande hizo mbili zilitia saini makubaliano ya siku saba kusitisha mapigano hapo tarehe 20 mwezi Mei yakilenga kuruhusu usambazaji wa misaada ya kibinadamu. Tarehe 29 mwezi Mei walikubaliana kuongezwa kwa siku tano.

Marekani na Saudi Arabia zinasimamia utekelezaji wa usitishaji mapigano na zimesema pande zote mbili zimekiuka.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana siku ya Jumatano katika kikao cha faragha kilichochukua muda wa dakika 90, kikao ambacho kiliitishwa na Katibu Mkuu Antonio Guterres. Ni mara ya tano tu katika kipindi chake cha zaidi ya miaka mitano kuomba mkutano kama huu.

Mji mkuu wa Sudan, Khartoum, umegubikwa na ghasia tangu tarehe 15 Aprili, wakati mapigano yalipozuka kati ya jeshi na vikosi vya Rapid Support Forces baada ya uhusiano kuvunjika kati ya kiongozi wa kijeshi Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na mkuu wa RSF Jenerali Mohamed Hamdan Degalo.

Majenerali hao wawili ni washirika wa zamani ambao kwa pamoja walipanga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021 ambayo yalivuruga kuundwa kwa serikali ya mpito ya utawala wa kiraia , baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir 2019.

Baadhi ya Taarifa za habari hii zinatoka katika mashirika la habari la AP na AFP.

Forum

XS
SM
MD
LG