Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Agosti 14, 2022 Local time: 21:09

Mgomo wa waendesha mashtaka Uganda watikisa mahakama


Rais Yoweri Museveni

Shughuli za mahakama zimeathirika nchini Uganda kufuatia mgomo wa wasimamizi wa mashtaka kote nchini, wakidai nyongeza ya mishahara pamoja na marupurupu mengine.

Wasimamizi hao wa mashtaka wamegoma baada ya kuipa serikali siku 14 kutekeleza matakwa yao.

Mwandishi wetu wa Idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa waendesha mashtaka hao wanataka nyongeza za mishahara.

Mbali na kutaka mazingira salama ya kazi, wasimamizi hao wa mashtaka wanataka kiwango cha mishahara kupandishwa kutoka shilingi 644,000 za Uganda hadi shilingi milioni 9, na mkuu wa mashtaka kupokea shilingi milioni 40 kutoka shilingi milioni 10 anazopata sasa.

Hii leo milango ya Mahakama ilikuwa imefungwa na waliofika kuhudumiwa walikosa huduma. Idara ya magereza na polisi nazo zimeathirika kutokana na mgomo huo.

Msemaji wa mahakama Solomon Muyita amesema: “Tumelazimika kusitisha shughuli za mahakama. Majaji hawawezi kufanya kazi bila wasimamizi wa mashtaka. Idhara ya mahakama imeathirika pakubwa na mgomo huu. Hakuna kuachiliwa washukiwa kwa dhamana hadi mgomo utakapomalizika”

Wasimamizi wa mashtaka pia wanataka idadi yao kuongezwa kutoka 300 wa sasa, kupata nyongeza ya marupurupu kwa kiwango cha asilimia 40, na kuruhusiwa kutolipa ushuru.

Vigezo wanavyozingatia katika kudai nyongeza ya mishahara ni kwamba wanafanya kazi katika mazingira hatarishi, wakilengwa na magaidi pamoja na mafisadi.

Mkuu wa mashtaka ya umma nchini Uganda Mike chibita amesema: “Tumeitisha mkutano utakaoshirikisha wahusika wote ili tujaribu kutekeleza baadhi ya matakwa ya wasimamizi wa mashtaka. Mkutano huo utaamua hatua itakayochukuliwa baadaye”.

Serikali, kupitia kwa Waziri Mkuu Dkt Ruhakana Rugunda, imeeleza Sauti ya Amerika kwamba Waziri wa Haki na Katiba Generali Kahinda Otafiire anashughulikia swala hilo, bila kutoa maelezo zaidi.

Lakini Rais Museveni amesikika mara kadhaa akionya kwamba atawafuta kazi wafanyakazi wa umma wanaogoma wakitaka kuongezewa mishahara.

Vyanzo vya habari nchini Uganda vimesema kuwa dereva katika mamalaka ya jiji la Kampala KCCA anapata mshahara mkubwa wa shilingi milioni moja, ikilinganishwa na Shilingi 644,000 anazolipwa msimamizi wa mashtaka nchini Uganda.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Uganda

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG